Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imeeleza na kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia ubora na kuhakikisha ujenzi unaendana na mahitaji ya soko.
Bodi hiyo imeeleza pia kwamba NHC ya sasa
inapaswa kuwa na uwezo wa kushindana na wawekezaji binafsi katika sekta ya
nyumba ili kufikia lengo la Serikali la kuwapatia watanzania makazi bora ya
kisasa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC, Dk. Sophia Kongela, ametoa hali hiyo baada ya ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya miradi ya Samia Housing Scheme Medeli, Njedengwa Valley View na Iyumbu Urban Apartments jijini Dodoma.
Ziara hiyo iliyowahusisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya NHC, imelenga kutathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, ubora wa ujenzi na namna Shirika linavyotekeleza dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa nyumba bora na za kisasa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Bodi imeridhishwa na mabadiliko yanayoonekana
katika utekelezaji wa miradi hii, pamoja na juhudi zinazofanywa na wahandisi na
Menejimenti ya NHC kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi inayotarajiwa,”
amesema Dk. Kongela na kusisitiza;
“Ukipita kwenye miradi ya NHC sasa unaona
kabisa nguvu kubwa iliyowekwa na kazi inayofanywa na wahandisi wetu.
Tunachotaka sasa ni kuona kasi hii inaendelea na suala la kuchelewa kuingiza
nyumba zetu sokoni lisiwepo tena.”
Kwa mujibu wa Dk. Kongela kasi ya ujenzi pekee haitoshi, bali nyumba zinazojengwa na NHC zinapaswa kuwa na ubora wa hali ya juu, usanifu wa kisasa na thamani inayoendana na matarajio ya wateja.
“Watu wa sasa wanataka vitu vizuri.
Ukilinganisha nyumba zetu na za waendelezaji wengine binafsi, NHC lazima iwe
katika viwango vya juu. Tunataka kutoa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na
kuzifikisha sokoni kwa wakati,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad
Abdallah, amesema Menejimenti ya shirika hilo limejipanga kutekeleza maelekezo
ya Bodi, huku hatua mbalimbali zikichukuliwa kuondoa changamoto zilizokuwa
zikisababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi hapo awali.
Amesema Shirika limeingia katika mikataba ya
muda mrefu na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi, hatua inayosaidia kuhakikisha
vifaa vinapatikana kwa wakati katika maeneo ya miradi na hivyo kupunguza
uwezekano wa kazi kusimama kutokana na uhaba wa vifaa.
“Katika maeneo yetu ya ujenzi hakuna uhaba wa
vifaa vya ujenzi. Timu zetu pia zinafanya kazi kwa kujituma sana; pale
inapohitajika, kazi zinaendelea hata nje ya muda wa kawaida ili kuhakikisha
ratiba zetu hazirudi nyuma,” amesema Abdallah.
Ameongeza kuwa katika baadhi ya miradi, utekelezaji wa kazi umefikia hatua ya kuwa mbele ya ratiba kwa takribani mwezi mmoja. Sambamba na hilo, NHC inaendelea kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa za ujenzi kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji huku ikidumisha viwango vya ubora.
Ziara hiyo ya Bodi ya Wakurugenzi wa NHC jijini Dodoma imeweka wazi mwelekeo mpya wa shirika hilo kwenda mbele kwa kasi, kujenga kwa ubora na kuhakikisha nyumba zinakamilika na kupelekwa sokoni kwa wakati, huku zikikidhi viwango na mahitaji ya soko la kisasa la makazi.
Kwa NHC, suala si kujenga nyumba pekee, bali ni kujenga kwa kiwango, kukamilisha kwa wakati na kuhakikisha mteja anapata thamani halisi ya fedha yake.







Chapisha Maoni