Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) Agosti 22 mwaka huu katika eneo la mradi Rufiji, mkoani Pwani.
![]() |
| Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi,(Aliyeketi mbele) akizungumza na waandishi wa habari. |
Amesema kuwa uzinduzi wa bwawa hilo ni tukio la kihistoria kwa Tanzania, likiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli za uzalishaji, uwekezaji na kukuza uchumi.
Waziri Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya kuzalisha umeme kuwahi kutekelezwa nchini, ukiwa umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452 na kutekelezwa kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
![]() |
| Bwawa la Mwalimu Nyerere linavyoonekana |
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, kwa sasa uwezo wa mitambo yote ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani MW 4,648, huku Kituo cha Julius Nyerere kikiwa na mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa umeme kwenye gridi ya Taifa.
Pia amesema hadi kufikia Mei 31, 2026, kituo hicho kilikuwa kimechangia takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingia katika gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja, hivyo kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya umeme nchini.
Waziri Ndejembi amesema tangu kuanza kuzalisha umeme, mradi huo umeendelea kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia katika gridi ya Taifa na kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa uzalishaji uliokuwa ukichangia mgao wa umeme.
Aidha, amesema bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, kiasi kinacholifanya kuwa rasilimali muhimu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, utalii na matumizi ya binadamu.
Amefafanua kuwa uwekezaji katika mradi huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na jitihada za Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha gridi ya Taifa na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi na uwekezaji.
“Mradi huu ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na uchumi wa Taifa,” amesema Ndejembi.


Chapisha Maoni