Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
WANAFUNZI 85 wanatarajia kwenda nchini India kuanzia wiki ijayo kwa ajili ya masomo, kupitia Wakala wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL).
![]() |
| Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel akizungumza na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda India kwa masomo kuanzia wiku ijayo. |
Wanafunzi hao na wazazi wao walihudhuria mkutano katika ofisi za GEL mwishoni mwa wiki, ambapo walipewa mafunzo kuhusu namna ya kuishi nchini humo, mambo ya kufanya na kutofanya, pamoja na masuala ya vibali, bima na makaazi.
Mbali na mafunzo hayo, wanafunzi hao walipewa tiketi za ndege, visa na nyaraka mbalimbali zitakazowawezesha kupokelewa katika vyuo wanavyokwenda kusoma. Wanatarajiwa kuanza kwenda India Agosti 21 na 23 mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel, aliwataka wanafunzi hao kulenga kupata GPA nzuri, lakini pia kutumia muda wao kutafuta fursa zitakazowasaidia baada ya kuhitimu.
“Tunahitaji GPA nzuri lakini pia huko kuna fursa nyingi sana. Mtasoma na watoto wa matajiri wenye viwanda, tunataka muwe karibu na watu kama hao kutambua fursa ya wewe kupata kazi, siyo unamaliza halafu unakuja kuhangaika kutafuta kazi wakati huko kulikuwa na fursa,” alisema.
Mollel aliwataka pia kuchagua marafiki wanaoongeza thamani katika masomo yao na kutumia fursa ya kukutana na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali kujifunza fursa zilizopo katika nchi zao.
Alisema India ina viwanda vidogo vidogo vinavyoweza kuanzishwa kwa mitaji midogo na kuwataka wanafunzi kuondokana na dhana kwamba kuanzisha biashara kunahitaji mabilioni ya fedha.
“India wameendelea sana kwa viwanda. Tumieni fursa hiyo ila isikutoe kwenye reli ya masomo yako. Jiulize unasoma kwa ajili ya GPA nzuri tu au unakwenda kuhamisha maarifa, kuchukua teknolojia na fursa za viwanda zinazopatikana kule kuleta hapa Tanzania,” alisema.
Amesema kuwa kila mwaka zaidi ya wanafunzi 800 hupitia GEL kwenda kusoma nje ya nchi na kwamba kuanzia mwakani taasisi hiyo itafungua fursa za ajira kwa kushirikiana na kampuni kubwa nchini zinazohitaji wataalamu mbalimbali.
Mollel amesema kuwa wanafunzi wanapaswa kuangalia pia fursa za ajira katika mataifa mengine, akitoa mfano wa Ulaya ambako kuna uhitaji wa rasilimali watu kutokana na watu wengi kustaafu.
“Ulaya kuna shida kubwa ya rasilimali watu kutokana na wengi kustaafu kwa umri. Sasa wewe ukisoma uhandisi jiongeze, soma na Kijerumani au Kifaransa, angalia lugha ambayo inaweza kukusaidia kupata ajira,” alisema.
Amesisitiza kuwa wanafunzi hao wasisome kwa ajili ya GPA pekee, bali warejee Tanzania wakiwa na maarifa, teknolojia na fursa zitakazowasaidia kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira.


Chapisha Maoni