ZIARA YA SAMIA URUSI YAFUNGUA MILANGO MIPYA YA BIASHARA, UWEKEZAJI

-Ukuaji wa biashara umefikia Dola milioni 307.5, uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 434 waonesha matokeo ya diplomasia ya uchumi Tanzania na Urusi

- Ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kukuza diplomasia ya uchumi na kutafuta masoko mapya ya bidhaa za Tanzania duniani

Mwandishi Maalum,Urusi

Wakati ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika Shirikisho la Urusi, ifungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ukuaji wa biashara kati ya nchi hizo unatajwa kufikia Dola za Marekani milioni 307.5 takriban shilingi 830.25 bilioni. 

Rais Samia Suluhu Hassan(kushoto), akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Vladmir Putin wa Urusi. Rais Samia yupo nchini Urusi wa ziara rasmi ya kiserikali.

Mbali na ukuaji huo wa biashara, uwekezaji unatajwa kufikia zaidi ya dola milioni 434 (Sh1.172 trilioni), huku ikielezwa ziara hiyo inafanyika kipindi ambacho uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na taifa hilo kubwa duniani yanaendelea kuimarika.

Katika miaka mitano iliyopita, ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili umeonyesha mwelekeo chanya, huku thamani ya biashara ikiongezeka kutoka dola za Marekani milioni 178.8(Sh483 bilioni), mwaka 2020 hadi kufikia takribani dola milioni 307.5 (Sh830.25 bilioni), mwaka 2025.

Ongezeko hilo linaakisi mafanikio ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza diplomasia ya uchumi na kutafuta masoko mapya ya bidhaa za Tanzania duniani.

Rais Samia Suluhu Hassan

Mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Urusi nayo yameendelea kuimarika, yakiongezeka kutoka dola milioni 7.5 (Sh20.25 bilioni), mwaka 2020 hadi dola milioni 29.5(Sh80 bilioni) mwaka 2025. 

Hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa za Tanzania katika soko la Urusi pamoja na kuimarika kwa ushindani wa bidhaa hizo kimataifa.

Bidhaa zinazopata nafasi kubwa katika soko hilo ni pamoja na chai nyeusi, tumbaku, korosho, nazi, maua ya waridi, ngozi, madini na bidhaa za mapambo ya mbao. 

Ukuaji wa mauzo hayo unachangiwa na ubora wa bidhaa za Tanzania pamoja na juhudi za kupanua masoko ya nje.

Kwa upande mwingine, Tanzania imeendelea kunufaika na bidhaa muhimu zinazoingizwa kutoka Urusi, ikiwemo mbolea, ngano, bidhaa za chuma, mafuta ya petroli, salfa na malighafi nyingine zinazotumika katika sekta za viwanda na kilimo. Bidhaa hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa ndani.

Mbali na biashara, ushirikiano huo umeendelea kuzaa matunda kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni za Urusi nchini. 

Hadi sasa, zaidi ya miradi 70 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22 imeanzishwa katika sekta tofauti za uchumi, ikizalisha zaidi ya ajira 3,018 kwa Watanzania na kuchangia uhamishaji wa teknolojia na ujuzi.

Miongoni mwa miradi hiyo, Mradi wa Uranium wa Mkuju River uliopo Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuvutia macho ya wawekezaji wa kimataifa. 

Mradi huo wenye thamani ya dola bilioni 1.2 unatekelezwa na Mantra Tanzania Ltd, kampuni tanzu ya ROSATOM ya Urusi, na unatarajiwa kuiweka Tanzania katika kundi la wazalishaji wakubwa wa uranium barani Afrika kwa uwezo wa kuzalisha hadi tani 3,000 kwa mwaka.

Faida zinazotarajiwa kutokana na mradi huo ni pamoja na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi, gawio na shughuli nyingine za kiuchumi zitakazochochewa na uwekezaji huo mkubwa.

Aidha, uzinduzi wa kiwanda cha majaribio cha uchakataji uranium katika eneo la Nyota mwaka 2025 na Rais Dk. Samia umeonekana kuwa hatua muhimu katika kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais Vladmir Putin wa Urusi.

Katika sekta ya nishati, ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaendelea kupitia miradi ya gesi asilia na gesi iliyoshindiliwa (CNG) inayotekelezwa kwa ubia kati ya Gazprom International na Anric Energy. Miradi hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi, nafuu na yenye uhakika kwa matumizi ya viwanda na wananchi.

Sekta ya usafirishaji nayo imeendelea kunufaika na ushirikiano huo. Kampuni ya FESCO, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), inaendelea na mipango ya kuboresha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam, ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu wa maendeleo ya gati namba 14 na 15. 

Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia zaidi ya tani milioni 30 za mizigo kwa mwaka.

Ziara ya Rais Samia nchini Urusi inaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Wataalamu wanaamini ushirikiano huo utafungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza biashara ya kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara, nishati na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi