WAZIRI DK.AKWILAPO:BODI MPYA NHC KAZIENI UKUSANYAJI MADENI, KULINDA UIMARA WA SHIRIKA

-Asema hakuna wa kuogopwa

-Asisitiza uwajibikaji aielekeza kuandaa mkakati unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuongeza tija ya uwekezaji wa makazi.

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, ameielekeza Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuimarisha usimamizi wa mapato na madeni ya shirika hilo, akisisitiza kuwa nidhamu ya kifedha ndiyo msingi wa kudumisha mafanikio na uimara wa taasisi hiyo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), jijini Arusha Juni 3, 2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC uliofanyika jijini Arusha, Dk. Akwilapo amesema Bodi hiyo inapaswa kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha wadaiwa wote wanatekeleza wajibu wao wa kulipa madeni kwa mujibu wa sheria, bila kupewa upendeleo wa aina yoyote.

“Msitishike linapokuja suala la kudai malipo halali ya Shirika. Hakuna mdaiwa anayepaswa kuogopwa au kupewa upendeleo. Wote watakiwe kulipa kwa mujibu wa mikataba, sheria na taratibu zilizowekwa,” amesema.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wa ufunguzi wa Bodi mpya ya wakurugenzi ya NHC, jijini Arusha Juni 3, 2026. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC Hamad Abdallah. 

Amebainisha kuwa NHC imeendelea kuwa miongoni mwa mashirika ya umma yaliyojijengea rekodi ya mafanikio katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara na uwekezaji, jambo ambalo limeiwezesha kubaki imara kifedha na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya makazi nchini.

Kwa mujibu wa Waziri Dk. Akwilapo, mafanikio hayo yanapaswa kulindwa kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha kila chanzo cha mapato kinatumika kikamilifu kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Dk.Akwilapo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa kwa NHC katika kuendeleza agenda ya makazi bora, miji endelevu na uwekezaji wa kimkakati unaochochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Waziri huyo pia ameitaka Bodi mpya  ya NHC kusimamia maandalizi ya Mpango Mkakati mpya wa Shirika utakaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo pamoja na malengo ya maendeleo endelevu yanayohusu makazi na maendeleo ya miji.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alisema Shirika limeendelea kuimarisha utendaji wake kupitia uwekezaji katika miradi ya makazi, biashara na matumizi ya teknolojia za kidijitali zinazorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli zake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hama Abdallah akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa shirika hilo jijini Arusha Mei 3,2026.

Alieleza kuwa NHC imeendelea kupanua vyanzo vya mapato kupitia upangishaji wa majengo, mauzo ya nyumba na viwanja, pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo tofauti nchini.

Hamad alisema Menejimenti ya NHC itaendelea kushirikiana kwa karibu na Bodi mpya ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi na kwamba shirika linaendelea kuwa taasisi ya mfano katika sekta ya makazi na uwekezaji wa mali isiyohamishika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC, Dk. Sophia Kongela, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiamini bodi hiyo na kuwapa wajumbe jukumu la kuendelea kuisimamia taasisi hiyo katika kipindi kipya cha utekelezaji wa majukumu yake.

Dk. Kongela alisema bodi imepokea kwa uzito maelekezo yaliyotolewa na Waziri na iko tayari kuyatekeleza kwa ushirikiano wa karibu na Menejimenti ya Shirika.

Alitaja maeneo yatakayopewa kipaumbele kuwa ni kuimarisha usimamizi wa mali za Shirika, kuongeza tija ya uwekezaji, kuboresha ukusanyaji wa mapato, kusimamia utekelezaji wa miradi ya makazi nafuu na kuhakikisha NHC inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya makazi nchini.

“Tunatoa hakikisho la ushirikiano wa karibu na Serikali pamoja na Menejimenti ya Shirika ili kuhakikisha NHC inafikia malengo yake na kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya makazi nchini,” alisema Dk. Kongela.

Uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC unaashiria mwanzo wa awamu mpya ya uongozi inayotarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa Shirika, kuimarisha uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya makazi bora kwa manufaa ya Watanzania, sambamba na kuchangia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi