-Lengo ni kuongeza ufanisi, kufanikisha utekelezaji Dira 2050
Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete amewahimiza Watumishi wa Umma kuendana na kasi ya maendeleo ya matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa pande zote za Muungano.
Ameyasema hayo leo jijini humo katika Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania 2026 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili nafasi ya utumishi wa umma katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unahitaji utumishi wa umma wenye uwajibikaji, ufanisi, ubunifu na uwezo wa kusimamia kwa mafanikio sera na mipango ya Serikali ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga imani kwa Serikali yao.
“Dira ya Taifa 2050 kwa Tanzania Bara na Zanzibar zimeweka msingi wa kujenga taifa lenye uchumi imara, linalotumia maarifa, ubunifu na teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu. Mafanikio ya utekelezaji wake yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa utumishi wa umma wa kisasa na wenye tija,” amesema Mhe. Kikwete.
Amesisitiza kuwa umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Bandia (AI) katika kurahisisha utoaji wa huduma za umma, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.
Ameongeza kuwa pamoja na matumizi ya teknolojia, utumishi wa umma unatakiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuharakisha utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Pia amekitaka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) kuendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti tumizi na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuzalisha watumishi wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya utumishi wa umma
Awali, akizungumza Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kongamano hilo limeandaliwa kama jukwaa la kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuimarisha utendaji wa taasisi za umma katika mazingira yanayobadilika kwa kasi.


Chapisha Maoni