Mwandishi Maalum, Moscow
Rais Vladmir Putin wa Shirikisho la Urusi amesema nchi yake itaendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Tanzania kwa manufaa ya nchi hizo, ili kuimarisha ushirikiano wa maendeleo.
![]() |
| Rais Vladmir Putin wa Urusi(kulia), akisalimiana na mgeni wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya nchi hiyo. |
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, pichani chini, amesema taifa lake limekuwa likifuatilia kwa karibu mageuzi mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania na kuridhishwa na kasi ya maendeleo yake.
Putin amesema mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa na manufaa makubwa kwa mataifa yote mawili ambapo ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Urusi na Tanzania kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.Kwa upande wake, Rais Samia pichani juu, amesema ziara yake nchini Urusi ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwake binafsi na kwa taifa la Tanzania kwa ujumla.
“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili, pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu. Kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa mwaliko huu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amekumbusha mchango mkubwa wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kumpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.
Rais Samia aliwasili jijini Moscow kwa ziara yake ya kwanza nchini Urusi, ambayo pia ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Tanzania nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, kwa ajili ya mazungumzo rasmi na Rais Putin.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi. Vilevile, walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yenye maslahi kwa mataifa yao.




Chapisha Maoni