ZIPA YAJIPANGA KUVUTIA UWEKEZAJI KIMATAIFA ZANZIBAR MKUTANO WA ZIS 2026

- Washiriki 500 kukutana na fursa zenye tija katika sekta za kimkakati zinazolenga utekelezaji wa Dira ya Zanzibar 2050, wamo wawekezaji wa kimataifa, wajasiriamali, washirika wa maendeleo

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Siku zinakwenda kasi kuelekea Mkutano wa Uwekezaji Zanzibar 2026 (Zanzibar Investment Summit – ZIS 2026), huku Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ikiongeza kasi ya kuvitangaza visiwa hivyo kimataifa, kuwa ni kitovu kipya cha uwekezaji ikiweka mkazo kwenye sekta zenye zinazolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.

Saleh Saad Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA

Mkutano huo, unaoratibiwa na ZIPA, umepangwa kufanyika Juni 3 hadi 5, 2026 ukitarajiwa kukutanisha washiriki kati ya 400 hadi 500  kutoka mataifa mbalimbali duniani, wakiwemo wawekezaji wa kimataifa, watunga sera, taasisi za fedha, viongozi wa biashara, washirika wa maendeleo, wajasiriamali pamoja na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji zitakazochangia sura mpya ya maendeleo ya Zanzibar.

Akizungumza kuelekea mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed, anasema maandalizi yanaendelea vizuri huku Zanzibar ikiendelea kujijengea mazingira ya kuvutia uwekezaji kupitia fursa zinazotekelezeka katika sekta mbalimbali muhimu.

Anaitaja kaulimbiu ya mkutano huo kuwa ni “Kukuza mseto wa uwekezaji kwa maendeleo endelevu Zanzibar: Kujenga simulizi jipya la ukuaji wa Zanzibar,” akieleza inaakisi dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha uchumi jumuishi, kuongeza ushindani wa uwekezaji na kupunguza utegemezi wa sekta chache za kiuchumi.

Saleh amesema mkutano huo unaofanyika wakati Zanzibar imeshaidhinisha miradi ya uwekezaji 1,351 yenye thamani ya Dola za Marekani14,291,020,523 takriban Shilingi 38.58 bilioni, hautakuwa tukio la kawaida bali jukwaa la kimkakati litakalowezesha visiwa hivyo kuonesha safari yake ya mageuzi ya kiuchumi na kuwaunganisha wawekezaji na miradi yenye tija inayoweza kuharakisha ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.

Kwa mujibu wa Saleh, ajenda ya mkutano huo imejengwa sambamba na Dira ya Zanzibar 2050 ambayo inaweka msisitizo katika uchumi wenye mseto, maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa sekta binafsi pamoja na kuongeza ushindani wa mazingira ya uwekezaji.

“Mkutano huu unatuma ujumbe wazi kuwa Zanzibar iko tayari kwa biashara na inakaribisha ushirikiano wa muda mrefu utakaosaidia kubadili sekta mbalimbali za uchumi na kuleta manufaa kwa wananchi,” amesema.

Sekta kadhaa zimeainishwa kama nguzo za mjadala na fursa kuu za uwekezaji katika mkutano huo, zikiwemo uchumi wa buluu, kilimo na biashara ya mazao, viwanda na biashara, mafuta na gesi, uchumi wa kidijitali, ubunifu, maendeleo ya miundombinu pamoja na utalii endelevu.

Katika eneo la uchumi wa buluu, Zanzibar inalenga kuvutia uwekezaji katika uvuvi wa kisasa, ufugaji wa viumbe baharini, usafirishaji wa majini, uchakataji wa mazao ya bahari kama mwani pamoja na teknolojia za uhifadhi wa mazingira ya bahari.

Sekta ya kilimo na biashara ya mazao nayo inatajwa kuwa na nafasi kubwa ya uwekezaji, hasa katika kuongeza thamani ya mazao, usindikaji wa bidhaa za kilimo, usalama wa chakula, uzalishaji wa mazao ya kuuza nje na teknolojia za kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Katika sekta ya viwanda na biashara, fursa zinatarajiwa kujikita katika uzalishaji wa bidhaa, minyororo ya ugavi, usafirishaji wa mizigo, maeneo maalumu ya viwanda pamoja na ujumuishaji wa masoko ya kikanda ili kuongeza ushindani wa uchumi wa Zanzibar.

Aidha, sekta ya mafuta na gesi pamoja na nishati inatarajiwa kuvutia wawekezaji wanaotafuta fursa katika usalama wa nishati na matumizi endelevu ya rasilimali.

Uchumi wa kidijitali nao umepewa uzito mkubwa kupitia majadiliano yatakayohusu miundombinu ya TEHAMA, teknolojia za kifedha (fintech), huduma za kidijitali, vituo vya ubunifu na mifumo ya kusaidia ujasiriamali wa kisasa.

Miundombinu inatajwa kuwa moja ya maeneo muhimu ya uwekezaji, ikijumuisha usafiri, bandari, barabara, maendeleo ya miji, huduma za msingi na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kuimarisha msingi wa ukuaji wa muda mrefu wa uchumi.

Utalii endelevu, ambao ni nguzo kuu ya uchumi wa Zanzibar, pia utaendelea kuwa eneo muhimu la uwekezaji huku mamlaka zikielekeza nguvu katika kuboresha huduma za ukarimu, kupanua utalii wa mazingira na kuvutia uwekezaji wenye thamani kubwa unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Mbali na kuonesha miradi ya uwekezaji, mkutano huo unatarajiwa kuonesha maboresho ya sera na mifumo ya udhibiti yatakayorahisisha mazingira ya biashara na kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Kwa wawekezaji wanaotafuta masoko mapya yenye ukuaji, Zanzibar inaonekana kujijenga upya kutoka uchumi unaotegemea zaidi utalii kwenda uchumi wenye mseto unaotegemea ubunifu, ushindani, ustahimilivu na maendeleo endelevu ya muda mrefu.

Mkutano huo Zanzibar Investment Summit 2026 ni hatua muhimu ya kuandika sura mpya ya uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo ya visiwa vya Zanzibar.

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi