Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuibua mijadala chanya kuhusu maadili lengo likiwa kukuza na kuimarisha uadilifu wa viongozi wa umma nchini, huku Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF),likitoa wito wa kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Maadili ili kuruhusu taarifa za mali za viongozi wa umma kuwa wazi kwa wananchi.
Pande hizo mbili zimetoa mapendekezo hayo kwa nyakati tofauti kwenye mkutano uliowakutanisha jijini Dar es Salaam Juni19,2026.
Kamishna wa Maadili, Jaji Sivangilwa Mwangesi, ametoa wito huo katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu wa Idara ya Uchunguzi wa Maadili, Kassim Mkwawa, kwenye ufunguzi wa mkutano wa Sekretarieti hiyo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambapo amesema wahariri na wanahabari kwa ujumla ni wadau muhimu katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi, kwa kuwa wanatumia weledi katika kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa kwa wakati.
“Wahariri wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla ni wadau wetu muhimu sana kwa sababu wanatumia weledi katika kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa kwa haraka na kuishawishi jamii kufikia lengo husika,” amesema.
Amesema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, semina, maonesho, makongamano na mikutano ya hadhara, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini na kwamba kila mdau anapaswa kujiuliza nafasi yake katika kukuza maadili na uadilifu nchini kupitia majukumu anayoyafanya.
“Kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza ni namna gani anachangia kukuza uadilifu nchini kupitia chombo chake anachofanyia kazi? Je, kuna vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili anavyokutana navyo katika utekelezaji wa majukumu yake? Naomba kila mmoja wetu ajitafakari, katika utendaji wake wa kazi anasaidiaje kukuza maadili ya viongozi?” amesema Mkwawa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Maadili ili kuruhusu taarifa za mali za viongozi wa umma kuwa wazi kwa wananchi, hatua aliyosema itasaidia kupunguza sintofahamu katika jamii.
Balile amesema kuwepo kwa uwazi wa mali za viongozi kutasaidia kuondoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya viongozi mbalimbali.
“Tukiendelea na sheria ya sasa, viongozi watazidi kusingiziwa kuhusu mali wanazomiliki. Ukipita mtaani utasikia mali hii ni ya kiongozi fulani hata kama si yake. Ili kuondokana na mambo haya, tunahitaji sheria iruhusu kiongozi wa umma mali yake iwe inafahamika wazi,” amesema Balile.
Amewataka wananchi kutambua kuwa Tanzania inaendelea na jitihada za kupunguza umasikini wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, hivyo si sahihi kumtuhumu kila kiongozi mwenye mali halali kuwa ameipata kwa njia isiyo sahihi.











Chapisha Maoni