-Zaahidi kushirikiana katika ubunifu, usanifu wa majengo na matumizi bora ya ardhi ili kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi
-Upungufu wa nyumba za makazi unakadiriwa kuwa nyumba 3,000 kwa mwaka
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) yameendelea kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya makazi nchini yakiahidi kushirikiana zaidi katika kubadilishana uzoefu, utaalamu na mbinu za kisasa za utekelezaji wa miradi ya nyumba na biashara ili kukidhi mahitaji ya makazi yanayoongezeka nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema hatua iliyofikiwa sasa si ya upande mmoja kwenda kujifunza pekee, bali ni ushirikiano wa kitaalamu unaozifanya taasisi hizo kuwa washirika wenye maono yanayofanana katika maendeleo ya sekta ya makazi.
“Awali kulikuwa na ziara nyingi za kujifunza, lakini sasa tunabadilishana uzoefu. Hii inaonesha namna taasisi zetu zilivyokua kitaalamu na uwezo tulionao katika kuendeleza sekta ya makazi,” amesema Hamad.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Sultan Said Suleyman, amesema NHC na ZHC ni taasisi zinazofanana kwa dhamira na majukumu, jambo linaloufanya ushirikiano wao kuwa muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto za makazi zinazotokana na ongezeko kubwa la watu mijini.
“Sisi ni kama mapacha. Tuna mengi yanayofanana, tuna changamoto zinazofanana na tuna mengi ya kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora,” amesema Sultan.
Viongozi hao wameeleza kuwa moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni matumizi bora ya ardhi kupitia ujenzi wa majengo ya kisasa yanayotumia nafasi kwa ufanisi mkubwa, hasa katika maeneo yenye uhaba wa ardhi kama Zanzibar na baadhi ya miji mikubwa Tanzania Bara.
Katika ziara za pamoja zilizofanyika kwenye baadhi ya miradi ya nyumba, viongozi na wataalamu wa taasisi hizo walijadili namna ya kuboresha usanifu wa majengo ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya maeneo ya ndani ya majengo pamoja na kuongeza thamani ya uwekezaji.
Hamad amesema baadhi ya miradi waliyoitembelea Zanzibar imeonesha ubunifu mkubwa katika usanifu wa majengo, hususan katika kuhakikisha kila eneo la jengo linatumika kwa tija.
“Moja ya mambo muhimu kwenye miradi ya makazi ni ufanisi wa matumizi ya nafasi. Tuliona usanifu wenye ubora mkubwa na matumizi mazuri ya maeneo ya ndani ya majengo,” amesema.
Viongozi hao, pia wamekubaliana kuwa kasi ya ongezeko la watu na ukuaji mahitaji ya makazi vinaifanya sekta hiyo kuwa agenda muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Sultan, Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya ongezeko kubwa la watu, huku eneo la ardhi likiwa dogo, hali inayolazimu taasisi za nyumba kuongeza kasi ya ujenzi wa majengo ya ghorofa na miradi ya kisasa ya makazi.
“Mahitaji ya makazi yanaongezeka kila siku. Hatuwezi kuendelea kujenga kwa mtindo wa zamani pekee. Lazima twende juu kwa kujenga majengo ya kisasa na kutumia ardhi kwa ufanisi zaidi,” amesema Sultan.
Viongozi hao pia wamezipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira mazuri ya kuendeleza sekta ya makazi nchini.
Wamesema dhamira ya viongozi wakuu wa taifa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia makazi bora ni fursa muhimu, ambayo taasisi za nyumba zinapaswa kuitumia kwa kuibua na kutekeleza miradi yenye manufaa makubwa kwa jamii.
Kwa pamoja, NHC na ZHC zimeahidi kuendelea kushirikiana katika tafiti, ubunifu wa usanifu wa majengo, usimamizi wa miradi na kubadilishana utaalamu ili kuhakikisha sekta ya makazi inaendelea kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya Taifa.






Chapisha Maoni