Dk Mwinyi ajitenga uvunjaji Katiba Zanzibar

-Apiga marufuku mjadala wa yeye kuongeza muda madarani

Mwandishi Wetu, daimatznews.co.tz

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amejitenga na uvunjaji Katiba ya Zanzibar kwa kujiongezea muda wa kukaa madarakani, akisema hana nia ya kuongeza muda wa Urais wa visiwa hivyo.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi

Dk. Mwinyi amsema hayo leo Mei 23, 2026 alipokuwa akifungua Jukwaa la Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi

Amesema kwamba muda uliowekwa kikatiba unastahi kuheshimiwa na kuagiza kusitishwa mara moja kwa mijadala kuhusu suala hilo.

Dk. Mwinyi amesema kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo Baraza la Wawakilishi, kwamba kumekuwa na mijadala na mapendekezo ya kuongeza muda wa Urais badala ya miaka 10 iliyowekwa na Katiba ya Zanzibar.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa hana dhamira hiyo na kwamba mjadala huo hauna tija kwa nchi kwa sasa.

Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, viongozi wameapa kuilinda Katiba ya Nchi na kuwataka wananchi na viongozi kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa maendeleo ya taifa.

 ''Kipindi kilichobaki cha uongozi wangu kitakuwa cha utekelezaji mkubwa na wa kasi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla,'' amesema.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali haitakuwa tayari kuendelea kubeba mashirika ya umma yanayoshindwa kujiendesha na kuendelea kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.

Amesema bado kuna mashirika ya umma yanayolipwa mishahara na kuendeshwa kwa fedha za Serikali, jambo alilosema limepitwa na wakati, huku akiitaka taasisi hizo kujipanga na kujiendesha kwa tija na faida.

Dk. Mwinyi amesema Serikali itatoa muda kwa mashirika hayo kufanya mageuzi ya kiutendaji na yale yatakayoshindwa kujiendesha Serikali haitakuwa tayari kuendelea nayo.

Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kuendelea kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na miundombinu ya barabara ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uchumi wa kisasa na endelevu.

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi