-Yanunua magari ya kisasa yanayobaini hatari kabla ya ajali kwa teknolojia ya Laser
-Ni Ford Ranger maalum
-Uwekezaji utakaoongeza usalama, ufanisi huduma SGR.
Mwandishi Wetu,
daimatznews@gmail.com
Katika kuimarisha usalama wa reli ya kiwango
cha kimataifa (SGR), Shirika la Reli nchini (TRC), limenunua magari maalum yanayotimia
teknolojia ya laser kwa ajili ya kukagua na kufuatilia reli hiyo.
Moja ya magari maalum aina ya Ford Ranger yaliyonunuliwa na TRC kwa ajili ya ukaguzi wa reli ya SGR
Taarifa ya Kitengo cha habari na Mawasiliano imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Masanja akieleza shirika hilo limenunua magari hayo aina ya Ford Ranger, yenye mfumo wa Hi-Rail.
"Magari hayo pia yana uwezo wa kubaini hitilafu za reli na vihatarishi mbalimbali kwa haraka na usahihi zaidi kuliko njia za kawaida za ukaguzi zilizokuwa zikitumika awali," amesema Mhandisi Masanja.
TRC yataja sababu uwekezaji
huo
Kwa mujibu wa TRC, magari
hayo maalum yana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa haraka
na uimara wa hali ya juu, yakiwa pia na uwezo wa kubadilika kwa urahisi kutoka
barabarani kwenda kwenye mfumo wa reli.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya.
“Magari hayo yamefungwa vifaa maalum vya
magurudumu ya reli, hivyo kuyawezesha kufanya kazi barabarani na kwenye reli
kwa urahisi,” ameeleza Machibya.
Hali hiyo inatajwa kuwa sifa kubwa ya kipekee
inayoyafanya kuwa bora kwa doria za kawaida na kutoa majibu ya haraka pale
changamoto zinapotokea, zikiwa na nguvu kubwa inayoyawezesha kufanya kazi
katika maeneo magumu, kubeba vifaa na kusaidia shughuli ngumu za ukaguzi wa
reli.
Yatakavyoondoa ombwe la ukaguzi
TRC imeeleza kuwa magari
hayo ni majibu ya haraka yanayoweza kuwassiadia wakaguzi kufika maeneo yenye
changamoto kwa haraka zaidi, jambo linalotajwa kuwa litapunguza muda wa
kusimama kwa huduma na kuongeza usalama wa wasafiri.
Sifa nyingine ya magari hayo imetajwa ni kuwa
na uwezo wa kufanya doria umbali mrefu wa reli ya SGR, yakiwemo yenye mazingira
magumu kufikika.
“Teknolojia ya laser uliopo kwenye magari
hayo, unachunguza hali ya reli kwa kupima usahihi wa njia, kubaini shida yoyote
katika reli ambavyo haviwezi kuonekana kwa macho ya kawaida,” amesema Mkurugenzi mkuu wa TRC na
kuongeza:
“Inaweza pia kuimarisha usalama, kubaini mapema hitilafu kunasaidia kuzuia ajali, hata kulinda abiria na kuhakikisha huduma za reli zinaendelea kwa ufanisi.”
Teknolojia ya Laser ni
nini?
Katika teknolojia ya Reli
ya SGR, mifumo ya ukaguzi wa laser hutumia miale maalum yenye usahihi mkubwa
kupima hali ya reli na ubora wa uso wa njia, ikiweza pia kubaini hata hitilafu
ndogo sana katika mpangilio wa reli.
Kuhusu kasi, teknolojia hiyo inaelezwa kuwezesha
ufuatiliaji wa moja kwa moja, wakati gari linaendelea kutembea kwenye reli,
huku pia likitumika kubaini nyufa, maeneo yenye udongo dhaifu na hata
kufuatilia mifumo ya umeme wa juu wa reli.
Kauli ya TRC na wasafiri
Akizungumzia zaidi magari
hayo, Mkaguzi wa Njia wa TRC, Manyama Mazula amesema; “Haya siyo magari ya
usafiri pekee, bali ni macho yetu kwenye reli.”
Mtumiaji usafiri wa SGR mara kwa mara,
Akwilina Msangi anasema hatua hiyo ya TRC kununua magari hayo kunaongeza Imani
kuhusu usalama wa safari za abiria kwa SGR.
“Kujua kuwa TRC inaweza kubaini matatizo
kabla hayajatokea kunatufanya tujisikie salama zaidi,” amesema Msangi.
Msafiri mwingine aliyetambulika kwa jina la Zuberi Mkwama, amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kununua magari hayo, akisema yataendelea kuhakikisha usalama wa abiria pamoja na mizigo.
Taswira kubwa zaidi
Uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya TRC
katika kuendelea kuboresha na kuifanya reli kuwa ya kisasa kwa kuunganisha magari ya kisasa pamoja na
teknolojia ya laser katika ukaguzi wa reli, hali ambayo inaifanya Tanzania kuendelea
kuendana na viwango vya kimataifa vya usalama wa reli, hivyo kuhakikisha Reli
ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma inaendelea kuwa mhimili salama na wa
kuaminika wa usafiri wa Taifa.


Chapisha Maoni