LUKUVI 'AKATISHA' ZIARA YA WABUNGE NHC

 -Mkurugenzi NHC asema alishiriki mradi uiotembelewa leo

- Atajwa ni mbunge, waziri mkongwe zaidi

-Ni mwalimu, kioo kwa wabunge na wanasiasa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Kifo cha Mkongwe wa siasa nchini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, William Lukuvi kimeilazimu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), kukatisha ziara waliyoianza kwenye Mradi wa Samia Housing Scheme, Dar es Salaam inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Marehemu William Lukuvi

Taarifa ya kifo cha Lukuvi imetolewa leo, Machi 25, 2026 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan  ikieleza kuwa waziri huyo amefariki saa 1 asubuhi.

Lukuvi anayetajwa kuwa mbunge aliyekaa bungeni kwa kipindi kirefu zaidi kati ya wabunge wa sasa hadi alipofariki, anaelezwa amekutwa na umauti wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma, baada ya kupatwa na mshituko wa moyo.

Wakati taarifa ya kifo cha Lukuvi ikitolewa, PIC ilikuwa katika ziara yake katika miradi ya Samia Housing na Kawe 711, ambapo pia ilipangiwa kutembelea Mradi wa Morocco Square na Jadda Hotel.

Mkurugenzi Mkuu NHC, Hamad Abdallah akizungumzia kifo cha Lukuvi, leo Machi 25,2026 Dar es Salaam.

Akitangaza kuahirisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa amesema hatua hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu za Bunge ili kupisha taratibu za msiba. 

Kadogosa amesema Bunge limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mbunge mwenzao, huku akitoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Spika wa Bunge na Watanzania wote, akieleza kuwa Lukuvi alikuwa kiongozi muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, hasa katika masuala ya sera.

Akimzungumzia zaidi, Kadogosa amemtaja Lukuvi kuwa mbunge mkongwe na mzoefu zaidi ambaye wengi wa wabunge akiwamo yeye walikuwa wakimsikia alivyokuwa akiwajibika bungeni hata baadhi kushawishika kuingia bungeni kwa mfano wa Lukuvi.

Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa akitoa taarifa ya kuahirisha ziara ya Kamati yake leo Machi 25,2026

Naye mbunge wa Biharamuro Ezra Chiwelesa ambaye pia ni mjumbe wa PIC amesema kwa wabunge wengi, Lukuvi alikuwa kama kioo na mwalimu lakini pia kifo chake kimeacha majonzi kwa wabunge na watanzania wengi hasa wanachi wa Jimbo la Isimani

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema shirika limepokea kwa masikitiko taarifa hiyo na kutoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu. 

"Lukuvi amefariki wakati leo Kamati ya PIC inafanya ziara katika miradi ya NHC, wakati mradi huu wa Kawe 711 unaanza, Lukuvi alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na alisimamia kuanza kwa mradi huu," amesema Hamad na kuhitimisha:

"Hivyo NHC imepoteza kiongozi mwenye maono makubwa katika maendeleo ya ujenzi wa nyumba bora za kisasa nchini."


Taarifa zaidi soma hapa chini:



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi