TRC yaanza kuunganisha injini za treni za reli ya MGR

-Yaweka historia Afrika Mashariki

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kuunganisha injini za treni za reli ya Meter Gauge Railway (MGR) ndani ya nchi, hatua inayofanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kutekeleza mpango huo. 

Hatua hiyo imepongezwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.

Wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi wa kuunganisha injini hizo katika Karakana ya Reli ya Pugu jijini Dar es Salaam leo Machi 14,2026, kamati hiyo imeishauri TRC kuendelea kuimarisha ujuzi wa vijana wa Kitanzania wanaoshiriki katika mradi huo kwa kuwapatia mafunzo ya juu ya kiufundi ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo,Selemani Kakoso, amesema kuwa uwekezaji katika kuendeleza taaluma za mafundi wazawa utasaidia kuongeza utaalamu wa kiufundi, ubunifu pamoja na ufanisi katika sekta ya reli nchini.

Pia meiihimiza TRC kuweka kipaumbele katika kutoa ajira kwa vijana waliopata mafunzo hayo ili waendelee kuchangia maendeleo ya shirika hilo pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kakoso ameipongeza TRC na Mkurugenzi Mkuu wake, Mhandisi Machibya Shiwa, kwa kile alichokieleza kuwa ni hatua ya kihistoria kwa Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, uamuzi wa kuunganisha injini hizo ndani ya nchi ulitokana kwa sehemu na ucheleweshaji wa upatikanaji wa vipuri kutoka kwa msambazaji SMH, uliosababishwa na changamoto za mnyororo wa usambazaji duniani kufuatia vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Kutokana na hali hiyo, TRC ilinunua injini mbili zikiwa zimekamilika kutoka Malaysia, huku sehemu nyingine za injini zikisafirishwa kuja Tanzania ili kuunganishwa katika karakana ya Pugu.

Mpango huo unaelewa kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ununuzi ambazo Serikali ingelazimika kutumia iwapo ingenunua injini zote zikiwa zimekamilika kutoka nje ya nchi. 

Mradi huo umefungua fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye ujuzi pamoja na kuwapa nafasi wasambazaji wa ndani wanaotoa vifaa na huduma mbalimbali za viwandani.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, pia ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya uchukuzi, akitaja upanuzi wa miundombinu ya reli pamoja na ununuzi wa vifaa vya uendeshaji kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha ufanisi wa sekta hiyo.

Amepongeza uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa zaidi ya kilomita 2,290 za reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) pamoja na ununuzi wa mabehewa na vifaa vingine vya uendeshaji ili kuongeza ufanisi wa usafiri wa reli.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, aliiambia Kamati ya Bunge kuwa mradi wa kuunganisha injini za MGR Class 91XX tayari umefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 34 wa Kitanzania ambao hapo awali hawakuwa na ajira.

Ameongeza kuwa mradi huo pia umefungua fursa kwa wafanyabiashara wa ndani wanaosambaza vifaa na huduma za kiufundi, ikiwemo kazi za uchongaji wa vyuma (machining), vifaa vya ujenzi, vifaa vya umeme, mabomba, vilainishi (lubricants), bidhaa za mpira pamoja na vipuri vingine vya viwandani.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi