Rostam Aziz ainunua NMG ya Kenya inayozalisha magazeti ya Daily Nation
- Arejea kwenye umiliki wa vyombo vya habari
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Mfanyabishara bilionea wa Tanzania, Rostam Azizi amenunua asilimia 100 ya hisa za Shirika la Aga Khan Fund for Economic Development S.A(AKFED), katika Kampuni ya Nation Media Group PLC(NMG), yenye makao makuu yake nchini Kenya, inayozalisha magazeti ya Daily Nation na kumiliki vituo mbalimbali vya redio na televisheni ukanda wa Afrika Mashariki.
![]() |
| Mtukufu Prince Rahim Aga Khan V (kulia) na mfanyabiashara wa Tanzania Rostam Azizi. Picha kwa hisani ya Mtandao wa Daily Nation. |
Bila ya kutaja thamani ya hisa, taarifa iliyotolewa leo Machi 10,2026 na AKFED imeeleza umiliki wake ulikuwa asilimia 54.08 ya hisa zote za NMG, ambazo sasa ni mali ya Rostam chini ya Taarifa Ltd, kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo wa Tanzania. .
Uamuzi huo wa Rostam kununua NMG, unamrejesha mfanyabiashara huyo bilionea wa Tanzania katika biashara, umiliki na uendeshaji wa vyombo vya habari, ambapo pia ni mmiliki wa Kampuni ya New Habari Corporation, iliyokuwa ikizalisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Dimba na The African ya hapa Tanzania hadi mwaka 2020 ilipofungwa.
NMG ndiyo kampuni inayomiliki Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inayomiliki magazeti ya Mwananchi, The Citizens na Mwanaspoti, ambayo waanzilishi wake walikuwa ni Rostam Azizi na Balozi Ferdnand Ruhinda ambaye sasa ni marehemu kabla ya kuuzwa kwa Aga Khan.
Hatua hiyo ya Rostam ni mwendelezo wa uwekezaji wake nchini Kenya na barani Afrika, ikikumbukwa kuwa mwaka 2024 bilionea huyo Mtanzania, Rostam Aziz, alitangaza ujenzi wa kituo cha gesi asilia ya kupikia (LPG) na eneo la kuhifadhia gesi hiyo katika mji wa Mombasa nchini Kenya, wenye thamani Dola za Marekani bilioni 1.9 sawa na takriban shilingi trilioni 4.55.
Taarifa zilieleza kuwa, mradi huo ni mwendelezo wa Kampuni ya Taifa Gas, inayomilikiwa na Rostam (pichani chini), kutanua wigo wa shughuli zake katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kusini, mbali na Tanzania.
Mwaka 2023, Rostam pia alitangaza kutanua uwekezaji wake kwa kufanya uwekezaji mpya, safari nchini Zambia wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 100 katika sekta ya nishati na madini.
Ilielezwa kuwa Rostam ambaye pia ni Mwenyekiti wa kampuni za Taifa Group inayofanya kazi ukanda wa Afrika Mashariki amefanya uamuzi wa kuwekeza fedha hizo, sawa na takriban shilingi bilioni 250, unaoashiria kuwa na mkakati wa kupanua zaidi wigo wa uwekezaji wake kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika.

Maoni
Chapisha Maoni