MAELEKEZO YA RAIS DK. SAMIA MRADI UJENZI MATENKI YA MAFUTA HAYA HAPA

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amezipa maelekezo maalum wizara na taasisi za Serikali akizitaka kuhakikisha Mradi wa Ujenzi wa Matanki ya Kupokelea na Kuhifadhi Mafuta eneo la Kigamboni, Dar es Salaam unatekelezwa kwa wakati na kukidhi viwango vya kimataifa.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Matanki ya Kupokelea na Kuhifadhi Mafuta eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, Machi 3, 2026.

Ameiagiza pia Wizara ya Nishati, kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya hifadhi ya mafuta na taifa linakuwa na akiba ya kutosha, ili kukabiliana na misukosuko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia, huku akieleza kwamba kupanda kwa bei ya mafuta duniani ni changamoto inayoongeza umuhimu wa kuwa na miundombinu madhubuti ya nishati.

Rais Dk. Samia ametoa maelekezo hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa kimkakati, Machi 3, 2026, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kwamba uwekezaji huo ni hatua muhimu ya kuimarisha nafasi ya Tanzania ambayo ni kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi za ukanda na kimataifa.

Amesema kwamba jiografia ya Tanzania inaipa fursa ya kuhudumia nchi zisizo na bandari akieleza kwamba Serikali imedhamiria kuitumia vyema fursa hiyo.

Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia maboresho yanayoendelea katika sekta ya bandari, reli na barabara yameongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa zaidi hivyo kuongeza ushindani kimataifa, akabainisha kwamba hatua hizo zimechangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa taifa.

Kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi, Rais Dk.Samia amesema: "Uamuzi huo ulikuwa wa kimkakati, ulioleta tija kubwa katika kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa bandari."

"Fedha zilizookolewa katika eneo hilo zimeelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa matanki hayo ya mafuta," amesema Rais Dk. Samia

Katika maelekezo yake, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia ubora, usalama wa mazingira na muda uliopangwa.

“Mradi huu umetumia fedha nyingi za Watanzania, hivyo lazima ujengwe kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesisitiza Dk. Samia.

Rais Dk. Samia ameagiza kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya wizara husika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ili kuimarisha mifumo ya uhakiki na ufuatiliaji wa shehena za mafuta kuanzia zinapowasili bandarini hadi zinaposambazwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuziba mianya ya upotevu wa mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa na yenye uwazi. 

Amewataka wakandarasi na washauri wa mradi huo kuhakikisha wanatekeleza kazi kwa uadilifu, ubora na kwa wakati ili kuwezesha mradi huo kuanza kufanya kazi mapema mwaka ujao, huku akieleza matumaini yake kwamba utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara, ajira na mapato ya taifa.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uchukuzi nchini na kuahidi kuwa wizara yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo.

"Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mafuta na kuimarisha usalama wa nishati nchini," amesema. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema dhumuni kuu la mradi huo wa ujenzi ni kuongeza uwezo wa taifa kupokea na kuhudumia shehena za mafuta kwa ufanisi zaidi.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya bandari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya soko la ndani na nchi jirani, sambamba na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi