PADRI MACHIBYA AWAKUMBUSHA WAKATOLIKI THAMANI YA UHAI
Mwandishi Wetu,
Waumini wa Kanisa Katoliki nchini wamekumbushwa kuwa uhai huanza na pumzi ya Mungu, na kuwataka kuutumia wakati huu wa kwaresma kukumbuka kwamba kila uhai ni pumzi iliyotoka kwa Mungu.
Rai hiyo imetolwa na Padri Vedastus Machibula wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza,(Pichani Juu), ambaye kwa sasa yuko Masomoni nchini Hispania, katika Tafakari yake ya Kwaresma ambapo amesema Yesu Kristo alimwaga damu yake kwa ajili ya uhai, ili wanadamu kukombolewa.
Kupitia ujumbe huo, amewahimiza waamini wa Kanisa Katoliki kuitazama Kwaresma kama wakati wa kutafakari kwa kina juu ya thamani ya uhai akieleza kuwa uhai ni zawadi takatifu kutoka kwa Mungu, inayopaswa kulindwa na kuheshimiwa katika kila hatua ya maisha ya Mwanadamu.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, uhai ni kitu Kitakatifu ambacho asili yake ni Mungu pekee, tangu kutungwa mimba hadi kifo cha kawaida.
Damu ya Yesu Kristo msalabani ni ishara ya upendo na uthibitisho wa thamani ya kila uhai kwa mwanadamu.
"Maneno haya ya Kristo yatukumbushe kilio cha wale wasio na sauti ya kuutetea uhai wao, tuwape maji (uhai) badala ya siki (kukatisha uhai wao), " amesema Padri Machibula.
Amesema Kwaresma ni kipindi cha siku arobaini cha maandalizi ya Pasaka, kinachotawaliwa na sala, kufunga na matendo ya huruma.
"Ni safari ya kiroho ya toba na wongofu wa ndani, inayomualika Mkristo kurejea kwa Mungu kwa moyo wa unyenyekevu, kujitakasa na kuimarisha dhamira ya kuishi kwa kuheshimu na kulinda uhai kama pumzi ya Mungu," amehitimisha.

Maoni
Chapisha Maoni