NHC: WANANCHI CHANGAMKIENI FURSA UMILIKI MAKAZI YA KISASA SAMIA HOUSING KIJICHI

-NMB watembelea, wajionea fursa 

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail

Shirika la Nyumba la Taifa, National Housing Corporation (NHC), limeweka wazi kuwepo kwa fursa mpya za umiliki wa nyumba za kisasa kupitia Mradi wa Samia Housing Kijichi, wilayani Temeke Mkoa wa Dar es Salaam wakiwataka wananchi wakiwemo watumishi wa Benki ya NMB Plc kuichangamkia.

Kwa hatua hiyo, NHC limeendelea kufungua milango ya umiliki wa makazi ya kisasa kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa mradi huo, unaolenga kutoa nyumba bora, salama na zenye miundombinu ya kisasa kwa wananchi wanaotamani kumiliki makazi yenye hadhi.

Akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa maofisa wa NMB Bank Plc, kuhusu mradi huo Machi,7, 2026, Ofisa Masoko wa NHC, Thobiasi Kavishe, amesema mradi huo unatarajiwa kujumuisha takribani nyumba 260 zitakazojengwa katika majengo ya ghorofa aina ya G+4.

Kavishe amesema, nyumba hizo zimepangwa kwa kuzingatia mahitaji ya makundi tofauti ya wanunuzi.

“Kutakuwepo na nyumba zenye chumba kimoja cha kulala, vyumba viwili pamoja na vyumba vitatu vya kulala, ili kutoa chaguo pana kwa wateja kulingana na uwezo wao wa kifedha na mahitaji ya familia.” amesema.

Amefafanua kuwa mbali na ubora wa majengo, mradi huo pia umejumuisha huduma mbalimbali za kisasa zitakazorahisisha maisha ya wakazi wake.

Kavishe amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na jenereta kwa ajili kukabili kukatika kwa umeme, ofisi ya usimamizi wa majengo (facility management office), mfumo wa kisasa wa utupaji taka (garbage chute), pamoja na maeneo maalum ya maegesho ya magari.

Miundombinu mingine muhimu itakayokuwepo ni pamoja na chumba chenye mitambo ya kusukuma maji, matenki ya maji, mandhari ya bustani, miundombinu ya mawasiliano ya mfumo wa mawasilaiano ya kompyuta( ICT) na waya za data, pamoja na uwanja wa michezo kwa ajili ya watoto na familia.

Katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kumiliki nyumba hizo, Kavishe amesema NHC imeweka mifumo rafiki ya malipo kwa mteja anayenunua nyumba hizo ambayo ni pamoja na malipo ya mara moja (single payment), malipo ya awamu kulingana na maendeleo ya ujenzi (progressive payment), pamoja na mfumo wa mkopo wa nyumba (mortgage loan) kupitia benki washirika.

Amebainisha kuwa kupitia mfumo wa mortgage, mnunuzi anatakiwa kuanza kwa kulipa angalau asilimia 10 ya thamani ya nyumba anayoichagua, huku kiasi kilichobaki kikilipwa kupitia mkopo wa benki kwa makubaliano kati ya mteja na taasisi ya fedha.

Mradi wa Samia Housing Kijichi ni sehemu ya juhudi za NHC za kupanua upatikanaji wa makazi bora, ya kisasa na yenye miundombinu rafiki katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Pia unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya ujenzi na taasisi za kifedha ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kutimiza ndoto ya kumiliki nyumba.




 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi