TRC:USAFIRISHAJI MIZIGO SASA KWA CONTAINER CARRIERS SGR
-Mteja wa kwanza apata ofa
Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza rasmi usafirishaji wa makasha kwa kutumia reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ikibeba makontena 100 kwa safari moja.
Hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa biashara nchini, kupunguza msongamano wa mizigo bandarini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda mikoa ya kati ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi wa Usafirishaji wa TRC, Focus Makoye Sahani, aliyezungumza wakati wa kuanza safari ya treni ya kwanza ya makasha kutoka Pugu Dar es Salaam kuelekea Ihumwa mkoani Dodoma, ameeleza kuwa treni hiyo inasafiri umbali wa takribani kilometa 420 kutoka Dar es Salaam.
"Leo tumeongeza wigo wa biashara kwa kupakia makasha. Kama mnavyoona, treni yetu ya kwanza ya makasha kwenda Ihumwa, Dodoma, leo imeanza safari zake na tuna ofa ya kutosha kutoka kwa mteja wetu wa kwanza,” amesema Sahani.
Amebainisha kwamba hatua hiyo ni mwanzo wa usafirishaji wa makasha baada ya TRC kuanza kusafirisha abiria pamoja na mizigo mbalimbali ikiwemo kichele kuanzia mwezi Julai, pamoja na saruji inayopakiwa Pugu.
Ameeleza kuwa treni hiyo ina mabehewa 50 yanayobeba jumla ya makasha 100, huku mteja wa kwanza, ambaze ni GSM, akipata ofa ya kuanzia kwa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa Sahani, TRC imeanza upakiaji wa makasha katika eneo la Pugu, huku ikifanya maboresho ya miundombinu ikiwemo Malindi Yard karibu na eneo la Gerezani ili kuimarisha shughuli za upakiaji wa makasha.
Sahani amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo bandarini, sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu ya kuhakikisha uwepo wa Vituo vya Kontena vya Ndani (ICD) katika Morogoro, na Ihumwa .
“Tutakuwa na ICD Morogoro ambayo ipo kilometa 193 kutoka Dar es Salaam, ambako wateja wanaoelekea Mbeya na Iringa wataweza kuchukua mizigo yao. Lakini pia kuna ICD ya Ihumwa ”amesema.
Ameongeza kuwa safari ya kuelekea Morogoro huchukua muda mfupi, huku mzigo unaoelekea Dodoma ukishushwa katika ICD ya Ihumwa, ambako kuna eneo kubwa na miundombinu ya kutosha kuhudumia makasha.
Akitoa wito kwa wafanyabiashara, Sahani amewahimiza Watanzania kutumia usafiri wa reli ili kupunguza utegemezi wa malori kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, akisisitiza kuwa huduma ya reli ya Standard Gauge ni rahisi, salama na yenye ufanisi.
Hii ni mara ya kwanza kwa TRC kutumia container carries, toka ilipoanza usafirishaji wa mizigo kwa SGR Juni 27, 2025.
Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipokea jumla ya mabehewa 264 ya mizigo ya SGR Desemba 2024 ambapo kati ya hayo mabehwa 200 yakiwa ni ya kubebea makontena (containers carriers) na 64 ni ya kubebea mizigo isiyofungwa (loose cargoes).



Maoni
Chapisha Maoni