SIKU 100 ZA RAIS DK. SAMIA, NHC YAANDIKA HISTORIA MPYA
- Ahadi zageuka vitendo, NHC ikiimarisha sekta ya makazi
-Mapato ya Bilioni 137.12, miradi yakamilika kwa kasi
-Ubunifu wa kifedha, kidijitali waongeza ufanisi wa Serikali
Katika uongozi wa kisiasa wa sasa, kipimo cha thamani ya Serikali si
wingi wa ahadi kwa wananchi, bali ni uzito wa matokeo ya utekelezaji wake.
Serikali hupimwa kwa vitendo vinavyoonekana na vinavyogusa maisha ya watu wake ndani
ya muda husika.
Ndani ya msingi huo ndipo unapopimwa pia utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika siku 100 tangu kuanza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita, mwaka 2025.
Katika kipindi hicho kifupi, utekelezaji wa ahadi umejidhihirisha kama
kioo kinachoakisi dira ya taifa, uongozi wenye uthubutu, maamuzi ya haraka na
matokeo yanayoonekana wazi kwa Watanzania. Haikuwa hadithi ya takwimu pekee,
bali simulizi ya uwajibikaji, ufanisi na matumaini mapya.
Moja ya vielelezo vya mafanikio hayo ni sekta ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambalo limeonesha mabadiliko ya dhahiri katika utendaji na usimamizi wa mali za umma.
NHC ilivyotekeleza ndani ya siku 100
Katika siku hizo 100, NHC limekusanya mapato ya shilingi bilioni
137.12, sawa na asilimia 97 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/2025. Huu ni
uthibitisho kwamba usimamizi madhubuti wa mali za umma unaweza kuzaa matokeo
makubwa bila kuathiri wajibu wa kijamii wa taasisi.
Faida kabla ya kodi imefikia shilingi bilioni 58.86—asilimia 138 ya
lengo lililorekebishwa—ikiifanya NHC kuwa mfano wa taasisi za umma zinazoweza
kujiendesha kwa ufanisi wa kibiashara huku zikichangia ukuaji wa uchumi wa
taifa.
Aidha, shirika limelipa kodi na tozo mbalimbali serikalini zenye thamani ya shilingi bilioni 38.64, mchango wa moja kwa moja katika kuimarisha bajeti ya Taifa. Katika ukusanyaji wa kodi ya pango, limevuka lengo kwa kufikia asilimia 104.14, ishara ya kuimarika kwa nidhamu ya kifedha na usimamizi wa wapangaji.
Miradi ya makazi na biashara yashika kasi
Katika kuimarisha upatikanaji wa makazi bora, NHC imekamilisha nyumba
560 katika mradi wa Samia Housing Scheme – Kawe jijini Dar es Salaam, ambapo
wanunuzi 177 tayari wamekabidhiwa nyumba zao. Hii inaonesha dhamira ya Serikali
kuhakikisha makazi bora yanakuwa haki halisi kwa Watanzania.
Dodoma, mji mkuu wa nchi, umefaidika kwa kukamilika kwa nyumba 68 katika eneo la Iyumbu, huku mauzo yakiendelea. Hatua hii inaendana na mkakati wa kuifanya Dodoma kuwa mji wa kisasa unaokidhi mahitaji ya watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.
Majengo ya Serikali katika eneo la Mtumba nayo yamefikia asilimia 96.5 hadi 97.4 ya ujenzi, mengi yakianza kutumika. Hii inapunguza gharama za upangaji na kuongeza ufanisi wa utendaji serikalini.
Kwa upande wa miradi ya kibiashara, Morocco Square imekamilika kwa asilimia 100 na tayari inaingiza mapato. Mradi wa Kawe 711, unaojumuisha majengo 10 ya ghorofa 17 na nyumba 422, umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Aprili 2026—uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuchochea biashara, ajira na ukuaji wa miji.
Mikoani, miradi kama Zongomela Kahama Shops (Shinyanga) imefikia
asilimia 99, jengo la 2H Commercial & Residential (Morogoro) limekamilika,
huku Masasi Commercial Complex (Mtwara) na Mtanda Commercial Complex (Lindi)
zikifikia asilimia 85 ya utekelezaji.
Matunzo, ubia na ubunifu wa kifedha
Katika kulinda na kuongeza thamani ya mali za umma, NHC limekarabati
nyumba 2,667 kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8—hatua inayoongeza ubora wa
makazi, kuimarisha usalama na kupunguza gharama za muda mrefu.
Pia, miradi 21 ya ubia yenye thamani ya shilingi bilioni 351 inaendelea kutekelezwa, ikiakisi sera ya kushirikisha sekta binafsi katika kuharakisha maendeleo bila kuathiri maslahi ya umma, sambamba na marekebisho ya Sheria ya NHC ya mwaka 2025.
Kwa upande wa ubunifu wa kifedha, maandalizi ya uzinduzi wa Hati
Fungani ya Nyumbani (NHC Bond) yanaendelea, hatua itakayopanua vyanzo vya
mitaji ya ndani na kuwawezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja katika
uwekezaji wa sekta ya nyumba.
Mageuzi ya kidijitali nayo yamepiga hatua kupitia App rasmi ya NHC
inayorahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na
kupunguza malalamiko ya wananchi.
Kukabili changamoto kwa uthubutu
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto hazikukosekana—ikiwemo ucheleweshaji wa malipo katika baadhi ya miradi ya Serikali na madeni ya kodi ya pango ya shilingi bilioni 21.4 kutoka kwa wapangaji waliopo na waliokwishaondoka.
Tofauti kubwa imekuwa katika namna changamoto hizo zilivyoshughulikiwa:
majadiliano ya mikataba, malipo kwa awamu, kuvunja mikataba kwa wadaiwa sugu na
matumizi ya mifumo ya taarifa za mikopo (CRB). Hii ni ishara ya uongozi
unaokiri hali halisi na kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya Taifa.
Kwa jumla, siku 100 za utekelezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Sita
si simulizi ya maneno matamu, bali ni ushahidi wa matokeo yanayopimika na
yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Ni taswira ya taifa linalojengwa juu ya uwajibikaji, ufanisi na maendeleo jumuishi chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan—ambapo makazi bora, uchumi imara na taasisi zinazowajibika kama NHC vinakuwa nguzo kuu za safari ya Tanzania kuelekea ustawi wa sasa na vizazi vijavyo.
.jpg)


Maoni
Chapisha Maoni