TAMICO YAPENDEKEZA MABORESHO HALI ZA WAFANYAKAZI NHC

 -Mkurugenzi Mkuu NHC ajibu unafanyiwa kazi ndani ya miezi 6

-Ataka TAMICO ichukue ya NHC kama mfano bora

 Mwandishi Wetu, daimatzanews@gmail.com

Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati na Ujenzi (TAMICO), kimependekeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuufanyia maboresho Mkataba wa Hali Bora kwa Wafanyakazi wa shirika hilo uliopo kwa maslahi ya watumishi hao, huku Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah ikiahidi kufanyia kazi ndani ya miezi sita.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo leo, Februari 11, 2026 jijini Arusha

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TAMICO Taifa, Partenus Rwechungura, alipokuwa akitoa salam za chama hicho cha wafanyakazi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC kwa mwaka 2026, unaofanyika jijini Arusha.

 “Marejeo ya mkataba yanapaswa kuzingatia maboresho ya stahiki mbalimbali, ikiwemo posho za makazi (house allowance) na masuala mengine yanayogusa ustawi wa watumishi, ili kuhakikisha mazingira bora ya kazi na motisha endelevu,” amesema Rwechungura pichani chini.

 Aliongeza kuwa uongozi thabiti na unaojali ustawi wa watumishi ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma na kwamba lengo la pendekezo hilo ni kuimarisha ulinzi wa haki, stahiki na maslahi ya wafanyakazi.

Hata hivyo, katika hotuba yake ya kumkaribisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Leonard Akwilapo aliyekuwa mgeni rasmi kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo alijibu; 

Baadhi ya wafanyakazi wa NHC wakifuatilia Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo unaoendelea jijini Arusha.

“Mkataba wa hali bora hatujaukalia, tutaufanyia kazi ndani ya miezi sita kwa makubaliano na TAMICO tawi la NHC, nilishakutana nao Februari 3, 2026. Ninaomba TAMICO mchukue NHC kama darasa kwenye eneo hilo.” 

Hamad alimpongeza Rwechungura kwa kuendelea kusimama kidete kutetea maslahi ya wafanyakazi na kuhimiza mazungumzo yenye tija kati ya menejimenti na watumishi wa NHC, huku Rwechungura akipongeza hatua ya Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC, kutoa muda wa miezi sita kwa ajili ya maboresho ya mkataba huo akieleza ni hatua ya msingi na inaonesha utayari wa pande zote kujenga makubaliano yenye manufaa ya pamoja.

 

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi