Muhimbili yaitwa kuhudumia Jeshi Comoro

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Katika kile kinachoeweza kuelezwa kuendelea kupaa kwa ubora wa huduma za Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), Jeshi la Comoro limeialika hospitali hiyo nchini humo na kuangalia uwezekano wa menejimenti na MNH kuanzisha huduma za kibingwa na bobezi nchini Comoro.

Tayari uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili umefanya ziara ya kikazi nchini Comoro kwa mwaliko wa jeshi hilo la Comoro, hatua inayotajwa ni maandalizi ya kuanzisha ushirikiano wa kimkakati kwenye huduma za Hospitali ya Jeshi na sekta ya afya kwa ujumla nchini Comoro.

Mwaliko huo wa Jeshi la Comoro umeelezwa kuwa na lengo la kuanzisha ushirikiano utakaohusisha menejimenti ya hospitali, huduma za kibingwa na kibingwa bobezi, uboreshaji wa vifaa tiba, tiba shirikishi, pamoja na maeneo mengine muhimu yatakayochangia kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanajeshi na raia wa Comoro.

Kwenye ziara hiyo ujumbe wa MNH uliongozwa na Mkurugenzi wake Mtendaji wa Dk. Delilah Charles Kimambo, ambayo ilitoa fursa ya kufanyika mikutano ya kitaalamu baina ya MNH, Hospitali ya Jeshi la Comoro wakiwamo viongozi waandamizi wa jeshi hilo. 

Uongozi wa MNH umeeleza utayari wa kushirikiana na Hospitali ya Jeshi la Comoro katika kuboresha mifumo ya uendeshaji wa hospitali, kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo na uhamisho wa ujuzi, pamoja na kusaidia katika uanzishaji wa huduma za kibingwa ambazo kwa sasa hazipatikani nchini humo.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Muhimbili ulitembelea miundombinu ya hospitali na kukagua vifaa tiba vilivyopo, lakini pia kupata fursa ya kujadiliana kwa kina na wenyeji wao kuhusu hali ya utoaji wa huduma za afya na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, ukiongozwa na Balozi Saidi Yakubu uliingana na kuuongoza ujumbe wa MNH katika shughuli zote za ziara, huku Balozi huyo akisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuendeleza diplomasia ya afya na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Ziara hiyo inatajwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Tanzania na Comoro kwenye sekta ya afya, lakini pia katika kuimarisha uhusiano wa kindugu na kimkakati.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi