WAZIRI DK. AKWILAPO AWATANGAZIA 'VITA' WANAOHODHI ARDHI, AIPONGEZA NHC
-Atishia kutumia Sheria Namba 113 kunyang’anya waliokaa na viwanja bila kuviendeleza.
-Ahimiza ujenzi wa nyumba nafuu kukabili upungufu wa nyumba milioni 3.8
Mwandhishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, ameanza kukunjua makucha, akieleza atawanyang’anya ardhi wote wanaohodhi bila kuziendeleza kwa muda mrefu, huku akilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuendeleza maeneo inayomiliki kwa kujenga miradi mbalimbali, hata kuzalisha faida ya Sh bilioni 58 kwa mwaka uliopita 2025.
Amesema wapo baadhi ya watu wanahodhi ardhi kubwa kwa kuziweka benki bila kuziendeleza wakati kuna watu wenye uhitaji wa ardhi ya kufanya uwekezaji wa nyumba bora za kisasa na miradi mingine ya maendeleo jambo alilosema sio sawa.
Amelikumbusha
Shirika la Nyumba la Taifa wajibu wake kuhakikisha inafanya kila linalowezekana
kujenga kuwawezesha wananchi kupata nyumba bora na za kisasa kwa gharama nafuu
kwa kupunguza gharama za ujenzi.
“Suala la ujenzi wa nyumba bora za kisasa na gharama nafuu ni kipaumbele cha Serikali, kwa NHC mtambue kuwa kuna upungufu mkubwa wa nyumba za makazi nchini, unakifia nyumba milioni 3.8. Hii ni fursa ya biashara kwenu,” amesema Dk. Akwilapo na kuongeza;
“Wananchi wakiangalia NHC wanaona nyumba bora, wanaona timu ya ushindi kufikia ndoto za makazi bora. Punguzeni gharama za ujenzi, ongezeni jitihada kujenga nyumba bora za gharama nafuu kwa wananchi.”
Waziri Dk. Akwilapo amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa utendaji mzuri uliowezesha kupata faida ya shilingi bilioni 58.86 kwa mwaka 2025 akieleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya uongozi na wafanyakazi, na kwamba ni muhimu mshikamano huo ukaendelezwa.
Dk. Akwilapo amewahimiza wafanyakazi kuwa na subira katika kipindi cha miezi sita kilichotengwa kwa ajili ya maboresho ya Mkataba wa Hali Bora, akisisitiza kuwa taratibu za kisheria na kiutawala lazima ziheshimiwe kabla ya mkataba kuwasilishwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.
![]() |
| Baadhi ya wafanyakazi wa NHC wakifuatilia mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo leo Februari 11, 2026 jijini Arusha. |
Amesisitiza kuwa NHC ina wajibu mkubwa kwa Watanzania wa kuwapatia makazi bora na yenye gharama nafuu, jambo ambalo ni kipaumbele cha Shirika.
Waziri Akwilapo pia ameeleza kuwa Wizara yake ipo tayari kushirikiana na NHC kwa kuwezesha uratibu na taasisi nyingine ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika.
Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya mapato, kukusanya kodi na kudai madeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo, ili kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa Shirika.
Katika kuimarisha utendaji, Dk Akwilapo amehimiza kukamilishwa kwa miradi kwa wakati ili kupunguza uhaba wa makazi nchini, pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani ya usimamizi wa fedha ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato.
Alisisitiza pia kuimarishwa kwa utawala bora, kuondoa rushwa na uzembe, na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo uwazi na uadilifu.
Awali, akimkaribisha Waziri Dk. Akwilapo, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah amesema katika mwaka uliopita wa 2025 shirika hilo limezalisha faida inayofikia shilingi 58.86 sawa na asilimia 138 ya lengo huku pia mizania yake ikikua.
"Faida kwa mwaka 2026 ni sh bilioni 58.86 na mizania ya NHC imeendelea kukua na kufikia takriban shilingi 6.4 trilioni kwa mwaka huu wakati mwaka uliopita tulipofanya mkutano kama huu, ilikuwa shilingi bilioni 5.5," amesema Hamad.





Maoni
Chapisha Maoni