Nyenzo Kuu 3 Dira 2050 kuanza kuwasilishwa bungeni kesho
-Bunge kuzijadili kwa wiki nzima
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Tume ya Taifa ya Mipango inatarajia kuwasilisha Nyenzo Kuu Tatu za kuanza utekelezaji wa Dira 2050, bungeni mjini Dodoma kesho Februari 2, 2026.
![]() |
| Katibu Mtendaji wa NPC, Dk. Fred Msemwa |
Baada ya kuwasilishwa na kupokelewa, Bunge litazijadili kwa
muda wa wiki moja kabla ya kutoa uamuzi wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Februari Mosi, 2026
Katibu Mtendaji wa NPC, Dk. Fred Msemwa ameeleza hayo akizitaja nyenzo hizo kuwa
ni pamoja na Mpango Elekezi wa Muda Mrefu ambao ni wa miaka 25 kuanzia mwaka
2026/2027 hadi mwaka 20250/2051, Mpango Elekezi wa Miaka Mitano w mwaka
2026/2027-2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka
2026/2027.
“Nyenzo hizo zitawasilishwa bungeni na Serikali kupitia
Waziri wa Nchi (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo,” amesema Msemwa
aliyekuwa akitoa taarifa kwa umma kuhusu maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji
wa Dira 2050.
Huku akihimiza Kuhusu wananchi kufuatilia uwasilishwaji wa
nyenzo hizo, Dk Msemwa amesema ni muhimu kwa kuwa Dira 2050 imebeba matumaini
ya Watanzania wote na imeandikwa kuzingatia maoni yao jambo linaloongeza
umuhimu kwa wananchi kujua na kufuatilia mipango iliyoandaliwa ili kutekeleza
Dira yao.
Katibu Mtendaji huyo wa NPC amesema ni fursa ya pekee kwa
kila mwananchi kufuatilia kutokana na ukweli kwamba uwasilishwaji wake ni jambo
lisilotokea mara kwa mara na linaweza kutokea tena miaka 25 ijayo,
” Dira inasisitiza kuhusu ustawi wa pamoja na ushiriki wa
kila mmoja katika ujenzi wa Taifa, hii ni alama ya umoja iliyo na nia thabiti
ya kutomuacha yeyote nyuma. Ni muhimu kila mtanzania kuwa na taarifa kamili ya
kinachoendelea katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa, ” amesisitiza Dk. Msemwa.
Kwa mujibu wa Katibu huyo wa NPC, mipango hiyo imepitia
ngazi zote za uamuzi serikalini na kwamba itawasilishwa ili kutoa nafasi kwa
Bunge kuzijadili na baadae kufanya maamuzi.
“Tume pia imeandaa mwongozo utakaohakikisha Mamlaka za Serikali
za Mitaa yakiwemo majiji na manispaa zote, mikoa yote, taasisi za umma, idara
na wizara mbalimbali zinaongozwa vizuri katika kutafsiri na kuelewa matarajio
ya Dira 2050 kwa usahihi,” amesema Dk. Msemwa na kuongeza;
“NPC imeandaa mwongozo wa upangaji wa mipango ya taifa na katika
kuhakikisba mwongozo huo unaeleweka kwa wadau NPC imeshafanya semina na
viongozi kutoka halmashauri zote, wizara, idara na taasisi za umma, ili
kujadili mwongozo huo na kuwa na uelewa wa pamoja.”
Katila hatua nyingine, Dk. Msemwa ameeleza kuwa NPC ipo
katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa
tathmini, unaolenga kuleta mageuzi ya ufuatiliaji, unaozingatia zaidi matokeo
ya kazi na uwajibikaji utakaoanza kutumika pamoja na utekelezaji wa Dira 2050 baade
Julai 2026.

Maoni
Chapisha Maoni