Makamu wa Rais: Uhuru wa Mahakama ni dhamana ya haki, sio kinga ya uzembe

- Mahakama zageukia AI kuongeza ufanisi utoaji haki

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu na kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa ikitambua umuhimu wa Mahakama katika ujenzi wa Taifa.

Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi

Dk. Nchimbi pia ametoa rai kwa majaji na mahakimu akitaka uhuru wa Mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki na kwamba uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.

Amesema hayo, alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika leo Februari 2,2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma.

“Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwa kata zote nchini zisizo na  Mahakama za Mwanzo,” amesema Dk.Nchimbi.

Amesema Mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.

Kiongozi huyo amesema Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi, kukuza uwajibikaji na nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, ambao amesema ni msingi wa maendeleo endelevu.

 “Ni muhimu Mahakama, ikazuia migogoro inayoweza kuwa chanzo cha migawanyiko ya kijamii au kisiasa na kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti,” amsema Dk. Nchimbi na kuongeza;

“Mi muhimu kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma, pia kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.”

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wote kuheshimu tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania George Masaju amesema Mahakama inaendeleza na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake ili kuimarisha ufanisi.

“Kwa sasa Mahakama inajenga mfumo unaotumia Akili Unde (AI) kwa ajili ya kurekodi mwenendo wa kumbukumbu za mashauri na hukumu mahakama,” amesema.

 Amesema katika mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi wanapozungumza mahakamani mfumo huo utatafsiri lugha iliyotumika na kuiandika kwa lugha iliyokuwa imechaguliwa kuandika kwa wakati huo huo.

Jaji Mkuu Masaju amefafanua kwamba mfumo huo utakapoanza kutumika utaimarisha ufanisi wa utendaji wa Mahakama kwani kuchukua kumbukumbu za mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kuandika kwa mkono au kompyuta kunachelewesha na wakati mwingine kupotosha.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi