NHC YACHORA RAMANI MPYA YA UFANISI NA UWAJIBIKAJI 2026/2027

-Faida ya Sh58.86 bilioni yatoa msukumo wa mageuzi ya kimfumo, kiutendaji
-Waziri ataka kasi ya nyumba nafuu na uwekezaji wa kimkakati kuelekea AFCON 2027
-Baraza la Wafanyakazi lapitisha maazimio mazito ya mapato, mifumo na huduma
-Serikali yataka nyumba nafuu, uwekezaji wa kimkakati na uwajibikaji zaidi

 Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) uliofanyika jijini Arusha umeweka msingi imara wa hatua mpya za kiutendaji, uwazi na ukuaji endelevu unaolenga kuleta tija zaidi kwa shirika hilo.

Mkutano huo umeibuka na maazimio mazito 23 yanayolenga kuimarisha mapato, mifumo ya utendaji na ustawi wa NHC kwa ujumla. Badala ya kuwa mkutano wa kawaida wa tathmini, kikao hicho kimekuwa jukwaa la kuweka mikakati mipya itakayolifanya Shirika la Nyumba la Taifa liendelee kuwa mhimili wa makazi bora nchini.

Maazimio ya mageuzi na uwajibikaji

Katika kujenga msingi wa ufanisi wa ndani, Baraza lilipitisha hatua kadhaa za kimkakati. Kipaumbele kikubwa kiliwekwa kwenye makusanyo ya kodi na madeni ya pango, ambapo ilisisitizwa kuwa kodi ilipwe ndani ya siku saba za mwezi husika kwa mujibu wa mikataba. 

Mikataba ihuhishwe kwa wakati, huku madeni ya wapangaji wa sasa yakifuatiliwa kwa hatua stahiki na waliotoka kuingizwa kwenye mipango maalum ya malipo, hata kwa msaada wa vyombo vya kisheria inapohitajika.

Ili kuongeza mapato, Baraza liliagiza maeneo yote yaliyo wazi yapangishwe haraka kwa kutumia mbinu mbalimbali kama kubadili matumizi ya maeneo, kugawa sehemu, kutangaza kwenye vyombo vya habari na kuweka mabango ya “Space to Let”. Pia, kuandaliwa kwa andiko la miradi mipya ya kibiashara (business cases) kwa lengo la kupanua vyanzo vya mapato.

Katika eneo la mifumo, imesisitizwa kufanyika kwa usafishaji wa takwimu (data cleaning) ili taarifa za mfumo zilingane na hali halisi ya uwandani. Aidha, mfumo jumuishi wa Shirika uboreshwe ili kuakisi hisa za miradi ya ubia, kuruhusu maombi ya safari kufanyika kidijitali na kupokea taarifa zote za upangishaji bila vikwazo vya nyaraka ngumu.

Ukarabati, hati na miradi ya ubia

Baraza pia limeelekeza kuimarishwa kwa ukarabati na matengenezo, likisisitiza matumizi sahihi ya fedha za dharura kwa wakati na kwa ubora. Mikoa ilitakiwa kuwasilisha mipango ya ukarabati mkubwa ikiambatanisha taarifa za hali ya majengo, gharama na muda wa kurejesha gharama hizo.

Katika kuimarisha usalama wa mali, viwanja vyote visivyo na hati viharakishwe kupata umiliki rasmi. Miradi ya ubia isimamiwe kwa kuzingatia mikataba na michoro iliyoidhinishwa, huku hisa za Shirika zikisajiliwa kikamilifu kwenye mfumo.

Kuhusu majengo mapya, imesisitizwa kuwepo kwa mchanganyiko bora wa wapangaji (tenant mix) na kuwapangisha wale wenye uwezo wa kulipa na kutunza mali za Shirika. Aidha, makusanyo ya gharama za huduma za pamoja (service charge) yaanzishwe katika milki zenye wapangaji wengi kwa utaratibu utakaoafikiwa kwa pamoja.

Msisitizo wa nyumba nafuu na maadili

Baraza limekazia pia ujenzi wa nyumba za bei nafuu kama utekelezaji wa maelekezo ya Serikali, pamoja na kupunguza hoja za ukaguzi kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo kikamilifu. Kumbukumbu za shughuli zinazoakisi mazingira, jamii na utawala bora (ESG) zihifadhiwe, huku taswira ya Shirika na utu kwa wateja vikilindwa.

Masuala ya ustawi wa wafanyakazi hayakuachwa nyuma. Ilielekezwa kuboreshwa kwa huduma za chakula, samani rafiki kwa afya, pamoja na maboresho ya ofisi za baadhi ya idara. Pia, kufanyika kwa tafiti za ubunifu wa vifaa bora vya ujenzi, hususan katika eneo la kuzuia maji (waterproofing).

Serikali yatoa dira na matarajio

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, aliipongeza NHC kwa mafanikio ya mwaka 2025 yaliyoiwezesha kupata faida ya Sh bilioni 58.86—sawa na asilimia 138 ya lengo. Alisema mafanikio hayo ni ushahidi wa ushirikiano mzuri kati ya menejimenti na wafanyakazi.

Hata hivyo, ameweka bayana matarajio ya Serikali kwa Shirika hilo, akisisitiza wajibu wake katika kupunguza upungufu wa nyumba nchini unaokadiriwa kufikia milioni 3.8. Alitoa wito wa kupunguza gharama za ujenzi na kuongeza kasi ya miradi ya makazi nafuu ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Aidha, amelitaka Shirika kuwekeza jijini Arusha katika maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, akihimiza taasisi za umma kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na mashindano hayo.

Menejimenti; Wafanyakazi msingi wa mafanikio

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah(pichani chini), alieleza kuwa mafanikio ya Shirika yanatokana na nguvu ya wafanyakazi. Alibainisha kuwa mizania ya Shirika imekua kutoka Sh trilioni 5.5 hadi Sh trilioni 6.4, huku likitambuliwa kama miongoni mwa walipa kodi wakubwa na kushinda tuzo za ufanisi.

“Mafanikio ya mwaka 2025—ikiwemo mizania kukua kutoka Sh trilioni 5.5 hadi Sh trilioni 6.4 na kulipa kodi ya takribani Sh bilioni 38.5—yasingewezekana bila nidhamu, weledi na uwajibikaji wa watumishi,” amesema Hamad.

Ameahidi kushughulikia mapendekezo ya maboresho ya Mkataba wa Hali Bora kwa watumishi ndani ya miezi sita kwa kufuata taratibu za kisheria na mazungumzo ya pamoja. 

Awali, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC, Faida Napacho alitoa maelezo kuhusu mkutano huo na kutambulisha viongozi na wafanyakazi, kisha kumkaribisha Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa shirika hilo, Fatma Chillo, huku akieleza kuwa Shirika la Nyumba la Taifa limebahatika kuwa na wanawake katika safu yake ya uongozi wa juu.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa NHC, Fatma Chillo amemtaja Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  wa shirika hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu, Hamad Abdallah akisema ndiye injini ya mafanikio yote ya shirika hilo.


Kwa ujumla, mtiririko wa maazimio na kauli za viongozi umeonyesha dhamira ya NHC kujenga upya uimara wake wa ndani na kupanua mchango wake kwa Taifa.

Kilichobaki sasa ni utekelezaji makini wa maamuzi hayo ili Shirika liendelee kuwa injini ya makazi bora na maendeleo endelevu nchini

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi