Mkazi Kibangu 'amlilia' DC Ubungo utekeleaji amri ya mahakama
-Ni kuhusu mgogoro wa ardhi unaotishia mustakabali wake
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
MKAZI wa Ubungo Kibangu, Monica Mujuni, ameiomba Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando(Pichani), kuhakikisha amri ya mahakama inaheshimiwa na mgogoro wa mipaka unaohusisha nyumba yake unatatuliwa haraka.
Monica amesema anahitaji ufumbuzi wa dharura ili kurejesha sehemu ya ukuta wa nyumba yake uliobolewa na jirani yake, akisisitiza kuwa eneo hilo tayari lilishapimwa kisheria na ana hati halali ya umiliki.
Akizungumza leo, Monica alisema mvutano huo ulianzia ngazi ya kata kabla ya kufika mahakamani, ambako alishinda kesi hiyo. Alieleza kuwa baada ya ushindi huo, maelekezo ya kupima eneo lake yalitekelezwa na ndipo alipopatiwa hati ya umiliki.
“Eneo langu limepimwa, nina hati halali. Jirani yangu wa nyuma analazimisha kupita katika uwani kwangu. Usiku alibomoa sehemu ya ukuta wangu na akaweka geti upande wa kwake likielekea kwangu, katika sehemu aliyoharibu,” alisema Monica.
Ameongeza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo aliwahi kufika katika eneo hilo kusikiliza pande zote zinazohusika, ambapo alimkabidhi nyaraka zote zinazoonesha umiliki wa eneo hilo. Kwa mujibu wa Monica, Mkuu wa Wilaya aliahidi kuwa mgogoro huo utashughulikiwa.
“Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kwa sababu mahusiano yangu na jirani yangu siyo mazuri, na hali hii inanitia wasiwasi wa usalama,” alisema.
Kwa upande wake, Edgar Rweyemamu, mmiliki wa nyumba namba 42 inayohusika katika mgogoro huo, alisema suala hilo kwa sasa liko chini ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Alieleza kuwa nyaraka zote za umiliki tayari ziliwasilishwa, na wanasubiri wataalamu wa ardhi kufika eneo la tukio kwa ajili ya uhakiki.
“Kwa sasa tunasubiri maafisa wa ardhi waje waangalie ramani na hati. Wao ndio waliotoa hati, hivyo wataangalia uhalali wake na kutoa uamuzi,” alisema Edgar.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangu, Hamisi Kureva, alipoulizwa kuhusu mgogoro huo, alisema suala hilo tayari lilishavuka ngazi ya kata na sasa liko chini ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, hivyo hawezi kulizungumzia.
Juhudi za kumpata Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, kwa simu yake ya mkononi ili kupata ufafanuzi zaidi hazikufanikiwa, licha ya kupigiwa mara kadhaa bila kupokelewa.

Maoni
Chapisha Maoni