Jamhuri 'yakwaa visiki' kesi ya kusafirisha 'unga'
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kusafirisha kilo 70.89 za 'unga' umekwaa kisiki, Mahakama imegoma kupokea notisi ya kuongeza vielelezo nane kwa sababu ina mapungufu.
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya imemtia uamuzi huo baada ya upande wa utetezi kuweka pingamizi maombi ya Jamhuri.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Sharifa Majani, Chigbo Innocent, Omari Omari na Mandela Masawe ambao wanashtakiwa kwa makosa manne.
Shtaka la kwanza ilidaiwa kati ya Januari Mosi mwaka 2019 na Aprili 4,2023 maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na Kilimanjaro waliandaa gengeni la uhalifu kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.
Shtaka la pili kwa mshtakiwa wa kwanza na wapili wanadaiwa Aprili 24,2023 maeneo ya Kiluvya wilayani Kisarawe walikutwa wakisafirisha kilo 25 za heroine.
Shtaka la tatu kwa washtakiwa wote walidaiwa kati ya Aprili 20,2023 na Aprili 22, 2023 maeneo ya Kiluvya na Himo mkoani Kilimanjaro walikutwa wakisafirisha kilo 45.89 za heroine.
Katika shtaka la mwisho ilidaiwa mshtakiwa wa kwanza Sharifa alidaiwa kati ya January Mosi mwaka 2019 na Aprili 4 mwaka 2023 maeneo ya Kiluvya alijipatia nyumba yenye thamani ya Sh milioni 168 huku akijua nyumba hiyo ni zao la uhalifu la kusafirisha dawa za kulevya.
Baada ya washtakiwa kukumbusha mashtaka yao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Yahya aliomba Mahakama ikubali kupokea taarifa ya kuongeza vielelezo nane.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Yahya alidai waliwasilisha taarifa Februari 17 mwaka huu baada ya Februari 16 kubaini kuna hitaji la kuongeza vielelezo.
Maombi hayo yalipingwa na mawakili wa utetezi, Josephat Mabula, Marietha Molela na Alfred Haongo wakidai taarifa ina dosari.
Walidai kwa nyakati tofauti kwamba Ilipaswa ieleze vielelezo kwa shahidi yupi, atajwe jina lake na maelezo yake yawepo.
Pia walihoji muda waliobaini kwamba wanahitaji kuongeza vielelezo na kuwa baada ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali walitakiwa kujua mapungufu hayo na kuwasilisha taarifa.
Mahakama katika uamuzi wake ilikataa kupokea taarifa hiyo kwa sababu ilikuwa na dosari.
Jaji Isaya alisema katika taarifa chini maelezo ya shahidi hayaonekani yalikuwa ya nani na kuongeza kwamba maelezo hayo yangeambatanishwa, hata kutaja jina la shahidi wa nane.
"Taarifa haielezi ni shahidi yupi , taarifa hii inakataliwa kwa sababu ina mapungufu,"alisema Jaji Isaya.
Baada ya kutiwa maombi ya kwanza upande wa Jamhuri uliomba kuwasilisha taarifa nyingine wakidai ilikuwa na ufafanuzi uliokuwa unakosekana katika taarifa iliyokataliwa.
Akijibu Wakili Mabula alidai upande wa utetezi wanapinga taarifa hiyo kwa sababu Mahakama haina Mamlaka ya kusikiliza taarifa ya pili kwa sababu tayari ilishatoka uamuzi.
Wakili Mabula alidai Mahakama inakosa mamlaka ya kujadili tena suala hilo katika mwenendo huo huo wa kesi na kwamba hata angekuja Jaji mwingine angekosa mamlaka hayo.
Akijibu, Wakili Yahya amedai Mahakama ina Mamlaka ya kuangalia nini kimeelezwa katika taarifa ,hata kama wangejua kabla ya Februari 16, 2026 kuwa wanahitaji kuongeza vielelezo maombi hayo yangewasilishwa siku ya kusikiliza shauri kama walivyofanya.
Amedai kama kungekuwa na namna nyingine ya kuwasilisha taarifa hiyo wangefanya hivyo , aliomba taarifa ya kuongeza vielelezo nane ipokelewe kwani hakuna kifungu kinachoeleza lini taarifa itolewe.
Akichangia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Baraka Mgaya amedai hakubaliani na hoja kwamba Mahakama haina Mamlaka ya kujadili hoja hiyo na kwamba taarifa ya kwanza ilikataliwa kwa sababu haikufafanuliwa ili upande wa pili waelewe.
"Notisi ya sasa tofauti haifananj ya Ile ya kwanza , kifungu cha Sheria hakisemi hakuna nafasi ya kuwasilisha taarifa nyingine baada ya ile kwanza kukataliwa, tunaomba taarifa ipokelewe,"amesema.
Jaji Isaya baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili ameahirisha shauri hadi Machi 24 mwaka huu kwa ajili ya uamuzi wa kupokea taarifa ya pili ama la.
Mwisho

Maoni
Chapisha Maoni