HINDU ANG’ARA NHC YAMTUZA KWA KUUZA NYUMBA NYINGI
- Mauzo ya nyumba 16 yambeba
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, amemtunuku cheti na tuzo ya Mfanyakazi Bora wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bi. Hindu Mwema kutoka Kurugenzi ya Uendelezaji Biashara NHC, kwa kutambua utendaji wake wa kipekee katika mauzo ya nyumba.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC, Waziri alimpongeza Hindu kwa kuonesha kiwango cha juu cha uwajibikaji, ubunifu na ari binafsi, hatua iliyomwezesha kuuza nyumba 16, idadi inayozidi hata baadhi ya watendaji wa Idara ya Mauzo na Masoko.
“Mafanikio hayo ni ushahidi kuwa malengo ya NHC yanaweza kufikiwa pale ambapo mtumishi anafanya kazi kwa bidii na weledi,” amesema Dk. Akwilapo.
Amebainisha kuwa utambuzi wa watendaji bora ni mkakati wa kujenga ushindani chanya, kuongeza motisha na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji ndani ya taasisi za umma huku akiwataka wafanyakazi wengine kuiga mfano huo, ili kuendeleza mafanikio ya NHC.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alimpongeza Bi. Hindu na
kumshukuru Waziri kwa kutambua mchango wa watumishi wa Shirika.
Alisema
tuzo hiyo ni ishara kuwa NHC inathamini juhudi na matokeo, na akawahimiza
watumishi wote kufanya kazi kwa malengo, kwa nidhamu na kwa kuzingatia maadili
ya utumishi wa umma.

Maoni
Chapisha Maoni