NHC YAFIKISHA BUNGENI DIRA YA MAGEUZI, TEKNOLOJIA YA MAKAZI BORA
- Utafiti na nyumba nafuu zatajwa suluhisho la baadaye
-
Kamati ya Bunge yataka utafiti kwa vifaa, teknolojia za kisasa kupunguza
gharama za ujenzi
-
Enzi za Mwalimu Nyerere hadi Dira ya 2050, NHC yathibitisha uwezo wa taasisi za
umma kujitegemea na kuleta tija.
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limeweka wazi mkakati wake wa muda mfupi, wa kati na mrefu wa kuboresha upatikanaji wa makazi bora na ya gharama nafuu nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, likisisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa za ujenzi, utafiti wa kina wa vifaa mbadala pamoja na uendeshaji wa miradi kwa ufanisi wa kibiashara, unaolinda dhamira ya kijamii.
![]() |
Kamati
ya Bunge: Pongezi na maelekezo ya kimkakati
Baada
ya kupokea na kujadili taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava, amelipongeza Shirika la Nyumba la
Taifa kwa kazi kubwa na yenye matokeo chanya, hususan katika eneo la ujenzi wa
nyumba, usimamizi wa mali za umma na kuimarisha uwezo wake wa kifedha.
Mzava amesema Kamati imeridhishwa na mwenendo wa Shirika, lakini ikaelekeza kufanyika kwa utafiti wa kina zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa na vifaa mbadala vya ujenzi vitakavyosaidia kushusha gharama za ujenzi wa nyumba, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati.
“Mahitaji
ya makazi yanaongezeka kila siku. Suluhisho si kujenga nyumba nyingi pekee,
bali kujenga kwa gharama zinazomudu wananchi. Tunaitaka NHC kushirikiana na
taasisi za utafiti na wadau wa teknolojia kubaini njia mbadala zitakazopunguza
gharama bila kuathiri ubora,” amesema Mzava.
Ameongeza
kuwa Kamati iko tayari kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi pamoja na NHC katika kuboresha sera, mifumo na mazingira ya kisheria
yatakayowezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini.
Waziri:
Mageuzi ya teknolojia ni ajenda ya Serikali
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema Serikali inaunga mkono kikamilifu mwelekeo wa NHC wa kuwekeza katika teknolojia za kisasa za ujenzi na utafiti wa vifaa mbadala, akisisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora kwa gharama nafuu.
Waziri
huyo amesema Wizara itaendelea kushirikiana na NHC katika kuboresha sera na
kanuni zitakazohamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kuongeza
kasi ya ujenzi wa nyumba na kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.
“Serikali
inaiona NHC kuwa ni mshirika muhimu katika utekelezaji wa sera ya makazi.
Mageuzi ya teknolojia, ubunifu na usimamizi thabiti ndiyo nguzo za kufikia
lengo la nyumba bora kwa wote,” amesema Waziri huyo.
NHC
yajivunia historia na mchango wa kitaifa
Awali, katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, ameeleza kuwa Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1962 kupitia Sheria ya Bunge Na. 45, likiwa miongoni mwa taasisi za kwanza kabisa kuanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka mmoja baada ya Uhuru wa Tanganyika.
Kwa
mujibu wa Hamad, lengo la awali la NHC lilikuwa ni kuwapatia wananchi makazi
bora na salama, sambamba na kusimamia na kuendeleza mali za majengo ya Serikali
na wamiliki wengine, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa kodi na matengenezo ya
majengo.
Amefafanua
kuwa katika hatua za mwanzo, NHC liliwezeshwa kifedha kupitia ruzuku ya
Serikali (asilimia 47), mikopo ya Benki ya Nyumba na Serikali ya Shirikisho ya
Ujerumani Magharibi (asilimia 40) pamoja na mapato ya ndani (asilimia 13), hali
iliyoweka msingi wa Shirika kujitegemea hatua kwa hatua.
Mageuzi
ya kisheria na kuimarika kwa ufanisi
Hamad
amesema mwaka 1990 NHC liliundwa upya kupitia Sheria ya Bunge Na. 2 kwa
kuunganishwa na aliyekuwa Msajili wa Majumba (RoB), hatua iliyopanua majukumu,
rasilimali na wigo wa kiutendaji wa Shirika.
“Marekebisho ya mwaka 2005 yalilenga kulifanya Shirika liwe na ufanisi zaidi katika mazingira ya ushindani wa kibiashara, bila kupoteza dhamira yake ya msingi ya kutoa huduma kwa umma,” amesema Hamad.
Majukumu
ya NHC, mwelekeo wa kimkakati
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, NHC lina majukumu makuu mawili ya kisheria:
Kwanza, kujenga nyumba za makazi na majengo mengine kwa ajili ya kuuza au
kupangisha, pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi kwa mujibu wa mipango
iliyoidhinishwa na Serikali.
Pili, kuzalisha au kuwezesha uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, kusimamia miliki
zake na za wamiliki wengine, kufanya matengenezo na kukusanya kodi za pango.
Katika
utekelezaji wa majukumu hayo, NHC limeanza kuelekeza nguvu katika utafiti,
ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa za ujenzi, jambo linaloendana na
maelekezo ya Kamati ya Bunge.
Mafanikio
ya kifedha: NHC yavuka malengo kwa asilimia 138
Taarifa
ya kifedha iliyowasilishwa imeonesha kuwa NHC limeendelea kuimarika kiuchumi.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Shirika lilipanga kupata faida kabla ya kodi ya
shilingi bilioni 30.10, lakini kufikia Juni 30, 2025, lilikuwa limepata faida
ya shilingi bilioni 58.86, sawa na asilimia 138 ya lengo lililorekebishwa.
Aidha, gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.2 mwaka 2024 hadi shilingi bilioni 6 mwaka 2025, ishara ya mchango chanya wa NHC katika mapato ya Taifa.
Hamad
ameeleza kuwa thamani ya mali za NHC imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni
6.3, ikichangiwa na ongezeko la miradi ya ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara
na umiliki wa ardhi.
Nyumba
za gharama nafuu na miradi ya kimkakati
Katika
eneo la makazi, Hamad ametaja utekelezaji wa Samia Housing Scheme,
mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini unaotekelezwa
katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam na Dodoma, ukiwa na lengo la
kuwahudumia Watanzania wa kipato cha chini na cha kati.
Mbali na hilo, NHC linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa majengo ya wizara jijini Dodoma, hospitali, masoko, shule na majengo ya biashara, miradi ambayo imeongeza ajira, kuboresha mandhari ya miji na kuchangia mapato ya Serikali.
Ushirikiano
na dira ya 2050
Kwa
upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imehimiza
kuendelea kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, NHC na wadau wa sekta
binafsi ili kuhakikisha mageuzi ya sekta ya makazi yanakuwa endelevu.
Kwa
mwelekeo wa mwaka 2026 na kuendelea, NHC limeweka kipaumbele katika kukamilisha
miradi iliyosimama, kuanzisha miradi mipya, kutafuta ardhi ya gharama nafuu na
kuimarisha utafiti wa teknolojia za ujenzi, hatua zinazoendana na Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2050.
Kwa
ujumla, pongezi za Bunge kwa Shirika la Nyumba la Taifa si tu kutambua
mafanikio yaliyofikiwa, bali ni wito wa kuongeza kasi ya mageuzi, ubunifu na
usimamizi bora. Katika safari ya zaidi ya miongo sita, NHC limeendelea
kuthibitisha kuwa taasisi za umma zinaweza kujitegemea, kuwa na tija na kuwa
mhimili wa maendeleo ya Taifa, ambapo makazi bora yanakuwa haki inayofikika kwa
Watanzania wengi zaidi, si ndoto ya wachache.







Maoni
Chapisha Maoni