NHC yaendelea kugusa maisha ya jamii: Wajasiriamali Kinondoni wapapatiwa mashine za uzalishaji

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kudhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii kwa kukabidhi mashine ya kisasa ya kukamulia juisi kwa vikundi vya wajasiriamali wasioona katika wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam—hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuongeza thamani ya shughuli zao za uzalishaji.

Watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wakishusha mashine ya kutengenezea juisi ya miwa kisha kuikabidhi kwa kikundi cha wajasiriamali wenye ulemavu wa macho Kinondoni, Dar es Salaam. Mashine hiyo imetolewa na NHC kuwasaidia wajasiriamali hao waweze kujikimu kimaisha.

Akizungumza kwa niaba ya vikundi hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wasioona Kinondoni, Vitalis Mdoe, ameishukuru NHC kwa kuitikia ombi lao na kutoa msaada huo muhimu, akisema mashine hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa vikundi vinavyojihusisha na utengenezaji wa juisi kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa na hatimaye kipato.

"Tumeshukuru sana kwa ujio wenu na kwa moyo wa kujitolea wa Shirika la Nyumba la Taifa. Mashine hii ni jawabu la maombi yetu, na ni chachu kubwa ya maendeleo kwa vikundi vya wajasiriamali wa mali katika eneo letu," amesema Mdoe.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa NHC, Yahya Charahani, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ya shirika, inayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan vijana, wanawake na makundi maalumu, ili kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea.

"Tunayo imani kubwa kwamba mashine hii haitakuwa tu kifaa cha uzalishaji, bali itakuwa nyenzo ya mabadiliko ya maisha—ikisaidia familia, watoto kupata mahitaji ya msingi, elimu, na hata kuwa chachu ya kumudu gharama za maisha," amesema Charahani.

Ameongeza kuwa NHC imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kusaidia vikundi vya ujasiriamali wa mali kupitia miradi mbalimbali ya kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa vikundi kujipanga, kushirikiana na kutumia fursa zinazotolewa kwa uwajibikaji na uendelevu.

Wanufaika wa msaada huo wameahidi kuitumia mashine hiyo ipasavyo, kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa, na kuendelea kushirikiana na NHC pamoja na taasisi nyingine kwa ajili ya maendeleo yao na jamii kwa ujumla.

Kupitia msaada huu, NHC inaendelea kuonesha kuwa jukumu lake halishii kwenye ujenzi wa nyumba pekee, bali pia linagusa moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kuchochea uchumi wa chini, kuimarisha ujasiriamali na kujenga jamii imara na yenye matumaini mapya.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi