Mambo mapya NHC 2026 ikibeba matumaini mpya ya makazi bora nafuu kwa Watanzania

 - Ziara ya Waziri Dk. Akwilapo yakoleza kasi

- Naibu Waziri ataka watumishi NHC kuwa mfano kwa kumiliki nyumba

 Mwandishi Wetu, daimatzanews@gmail.com

Mwaka mpya, mambo mapya. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kipindi hiki dunia inapoanza mwaka mpya wa 2026.

Mambo hayo mapya kwa NHC yanabeba matumaini mapya ya makazi bora, nafuu kwa Watanzania yakibebwa na shirika hilo huku likijipanga kuongeza zaidi kazi ya utekelezaji miradi yake na tafiti ili kubuni na kupata matokeo chanya katika kutimiza majukumu yake kuwapatia wananchi nyumba bora.

Hayo yanabainika wakati wa ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, pamoja na Naibu wake Kaspar Mmuya, katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Januari 5, 2026, siku tano tu, baada ya kuanza mwaka mpya 2026.

Ziara hiyo iliyoandika historia imekuwa tukio lenye uzito mkubwa katika mwelekeo wa sekta ya makazi nchini.


Hii ni kutokana na ukweli kwamba ni ya kwanza kwa Waziri Akwilapo kujitambulisha rasmi katika shirika lililo chini ya wizara yake tangu alipoteuliwa, ikibeba ujumbe mzito wa sera, uongozi na matumaini mapya kwa Watanzania wengi wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa makazi bora na yenye gharama nafuu.

Kwa miaka 63 tangu kuanzishwa kwake, NHC imekuwa taasisi ya kimkakati katika utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yenye hadhi.

Hivyo basi, ujio wa Waziri na Naibu wake katika makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam unaashiria dhamira ya dhati ya Serikali kuimarisha nafasi ya NHC kama chombo kikuu cha kutafsiri sera za makazi kuwa uhalisia unaogusa maisha ya wananchi.

Katika hotuba yake kwa menejimenti na watumishi wa NHC, Dk. Akwilapo ametoa maelekezo ya wazi na yenye mwelekeo wa muda mrefu, akisisitiza umuhimu wa utafiti wa kina katika kubuni na kutekeleza miradi ya makazi.

Ameielekeza NHC kufanya tafiti zitakazowezesha ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kawaida. 

Kwa msisitizo, Waziri ameeleza kuwa unafuu wa gharama, lazima ueleweke kwa kuzingatia makundi tofauti ya Watanzania, hali zao za kiuchumi na mahitaji yao halisi.


Maelekezo hayo yameenda sambamba na wito wa kutumia teknolojia za kisasa na bunifu katika sekta ya ujenzi. 

Kwa mujibu wa Waziri Akwilapo, kupitia tafiti za kisayansi na ubunifu, NHC itaweza kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora, huku ikizingatia mazingira, hali ya hewa, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na mitindo ya maisha ya jamii mbalimbali.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za NHC katika utafiti na maendeleo (R&D), ikiwemo ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, wataalamu wa ujenzi na sekta binafsi.

Zaidi ya hilo, Waziri Dk. Akwilapo ameielekezata NHC kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi yake na kuepuka ucheleweshaji unaoongeza gharama.

Pia akaagiza NHC iimarishe ukusanyaji wa madeni

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk, Leonard Akwilapo

ya wateja wake, ili kuongeza mtaji wa ndani na uwezo wa kufikia malengo yake, akieleza matarajio yake kuwa ifikapo mwaka 2030, NHC itakuwa imechangia kikamilifu utekelezaji wa malengo ya Wizara na Serikali kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chama tawala.

Katika ujumbe uliogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, Waziri huyo ameeleza kuwa NHC ina uwezo wa kuwaondolea Watanzania mzigo wa ujenzi binafsi unaoambatana na changamoto za mafundi wasio waaminifu, gharama zisizotabirika na usimamizi mgumu wa miradi.

“Kwa kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu, NHC itasaidia kupunguza msongo wa mawazo unaowakabili wananchi wengi wanaojaribu kujenga makazi yao wenyewe,” amesema.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kasper Mmuya

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Kaspar Mmuya ametoa wito wa kipekee na wa kuhamasisha kwa watumishi wa NHC.

Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Dk. Akwilapo, Mmuya amewataka watumishi wa NHC kuwa mfano bora wa kuishi katika makazi bora kwa kujenga au kumiliki nyumba zao binafsi, ili kuonesha kwa vitendo mafanikio ya sera na mikakati wanayoisimamia kitaaluma.

Kwa msisitizo, Mmuya amesema; “Watumishi wa NHC wanapaswa kuishi kwa hadhi inayolingana na dhamana yao, nidhamu na ufanisi, badala ya kuwa watazamaji wa mafanikio wanayoyahubiri.”

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa NHC, Fatma Chillo 

Akitoa neno la shukurani, mbele ya Waziri wa Ardhi kwa niaba ya wafanyakazi wa NHC, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Fatma Chillo amesema, wamepokea na watatekeleza maagizo, ushauri na maelekezo kutoka kwa waziri huyo na naibu wake.

Awali, akizungumza mbele ya Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alimhakikishia kiongozi huyo kwamba shirika lake litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kuzingatia sera na miongozo yote ya Serikali.

“NHC inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi na biashara nchini kwa mwaka 2025 Shirika lilipata tuzo tatu tofauti kutokana na utendaji bora, ikiwemo ulipaji wa gawio kwa Serikali,” amesema.

Kwa mujibu Hamad, NHC imejipanga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili kutimiza wajibu wake katika kufanikisha ajenda ya makazi bora, salama na nafuu kwa Watanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah

Ziara ya Waziri Dk. Akwilapo na Naibu wake NHC imeacha taswira chanya ya ushirikiano imara kati ya Serikali na Shirika hilo lakini pia hamasa mpya katika kutekeleza majukumu ndani ya shirika hilo.

Ni ziara iliyoweka mwelekeo mpya unaosisitiza utafiti, ubunifu, uwajibikaji na kasi ya utekelezaji, ikiwa pia hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye makazi bora, miji iliyopangwa na maisha yenye heshima kwa wananchi wote.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi