Dk. Akwilapo aagiza NHC ifanye tafiti kupata suluhisho nyumba bora za gharama nafuu

 -Asema usimamizi wa ujenzi ni pasua kichwa kwa wananchi

- NHC inaweza kuwaondolea wananchi tabu hiyo

- Ataka watendaji wasiwe maafisa mchakato

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC), kufanya tafiti na kuja na jawabu la upatikanaji wa nyumba bora nafuu za kisasa kwa watanzania wenye kipato cha kawaida.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC),jijini Dar es Salaam leo, Jumtatu Januari 5, 2026.

Dk. Akwilapo ametoa agizo hilo leo Januari 5, 2026 Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salam, alipofanya ziara yake ya kwanza kujitambulisha katika shirika hilo pekee, lililo chini ya wizara yake, tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Fanyeni tafiti za nyumba za gharama nafuu kwa watanzania wa kawaida. Nawatuma mjenge nyumba bora za bei nafuu kwa ajili ya watanzania wenye kipato cha kawaida, Watanzania waingalia NHC,” amesema.

Mbali na kukutana na menejimenti ya NHC, Dk Akwilapo aliyeongozana na Naibu wake, Caspar Mmuya pia walizungumza na watumishi wa shirika hilo lenye miaka 63 tangu lilipoanzishwa.

 Waziri Akwilapo amesema NHC ina nafasi ya kuimarisha utafiti na ubunifu katika sekta ya ujenzi ili kubuni mbinu na teknolojia zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata nyumba bora, salama na zenye gharama nafuu.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC), Hamad Abdallah alipofanya ziara yake ya kwanza makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam leo, Januari 5,2026,

Ameeleza kuwa kupitia tafiti hizo za kisayansi na matumizi ya teknolojia bunifu, shirika hilo litaweza kubuni aina za nyumba na mifumo ya ujenzi kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa wananchi, hali ya hewa, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi pamoja na mitindo ya maisha ya jamii husika.

“Utafiti ni njia sahihi ya kupata suluhisho la kudumu. Tukifanya utafiti wa kutosha, tutajenga nyumba zenye ubora, gharama nafuu na zitakazowafikia Watanzania wengi zaidi,” amesema.

Waziri huyo ameiambia NHC kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za shirika hilo katika utafiti na maendeleo (R&D), ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, wataalam wa ujenzi na wadau wa sekta binafsi  ili kuongeza tija na ubunifu katika miradi ya makazi. Kwa mujibu wa Dk. Akwilapo NHC ina uwezo wa kutekeleza hilo hivyo kuwaondolea wananchi mzigo wa mawazo, hasara na kutapeliwa na mafundi wasio waaminifu wakati wa ujenzi kwa kuwajengea nyumba bora kwa gharama nafuu.

“Hakuna ‘stress’ kubwa kama kukutana na mafundi wa ujenzi, utaambiwa vifaa vya ujenzi bei hii kumbe, sivyo, utaambiwa gharama za ujenzi hizi, hazilingani na uhalisia, hata kusimamia mafundi ni kazi kubwa kwa mwananchi, wakati mwingine mafundi wapo matapeli;

Mkilifanya hilo, NHC mtawaondoa wananchi kwenye pasua kichwa hiyo ya ujenzi.”

Amewataka kufanya kazi kwa kuheshimiana na kuheshimu wananchi wanaofika kwenye ofisi za NHC kufuata huduma mbalimbali hasa makazi bora.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo (kushoto), akisalimiana na  Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Kaspar Mmuya wakati walipofanya ziara makao makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), jijini Dar es Salaam Januari Januari 5, 2026, Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah.

Amesema NHC ina dhima kubwa ya kuhakikisha hata wananchi wa kawaida wanapata nyumba bora, akisisitiza kufanya utafiti utakaokuwa mwarobaini na tatizo la makazi.

Amewaonya akiwataka wasiwe maofisa michakato, ambao kila wanapokutana na wateja wanawaeleza jambo husika bado lipo kwenye mchakato.

Waziri Dk. Akwilapo pia ameiagiza NHC kuendelea na kasi ya utekelezaji miradi yake na kuepuka kuichelewesha ili kukwepa kuongeza gharama ya miradi hiyo, akilitaka pia lifanye upembuzi yakinifu ili kuongeza majengo mengine mbali na makazi.

Baadhi ya watendaji wa NHC wakifuatilia mkutano wao na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo uliofanyika makao makuu ya shirika hilo, Dar es Salaam Januari 5, 2026.  

“Shirika liongeze kasi ya kukusanya madeni ya wateja wake, ili fedha ziliwezeshe NHC kufikia malengo yake,” ameagiza Dk. Akwilapo na kungeza;

"Matarajio yangu ifikapo mwaka 2030, NHC inafikia malengo yake katika kutekeleza malengo ya Wizar ana Serikali kama yalivyoongozwa na Ilani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, (CCM)."

Dk. Akwilapo ameipongeza menejimenti na wafanyakazi wa NHC kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwenye utekelezaji wa agenda ya Serikali ya kuwapatia Watanzania makazi bora, salama na yenye hadhi, akiweka wazi kuwa mafanikio ya Shirika hilo yanaakisi uwajibikaji, weledi na uzalendo wa watumishi wake.

“NHC ni taasisi muhimu katika kutafsiri maono ya Serikali ya makazi bora kuwa uhalisia. Mafanikio mnayoyapata ni ushahidi wa kujituma na ufanisi wa wafanyakazi wake,” amehitimisha.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, akizungumza na watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kabla ya kumkaribisha Waziri wake kuzungumza na hadhara hiyo Januari 5,2026.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewataka wafanyakazi wa NHC kuwa mfano bora wa kuishi katika nyumba bora za makazi, ikiwemo kujenga au kumiliki nyumba zao binafsi, ili kuonesha kwa vitendo kile wanachokisimamia kitaaluma na kujimudu kiuchumi.

Amesema watumishi wa NHC wanapaswa kuwa kielelezo cha mafanikio ya sera na mikakati ya makazi bora, huku wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi, nidhamu na heshima.

Watumishi wa Shirika la Nyumba la Taifa, wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo(Hayupo pichani), wakati waziri huyo alipofanya ziara makao makuu ya NHC.

" Sategemei kuona wafanyakazi wa NHC wakiwa na tabia ya kama ya 'wapiga debe,' wa daladala, wanahamasisha wengine kupanda magari ya umma huku wao wakiachwa vituoni, badala ya kuwa mfano wa kujimudu na kupanga maisha yao kwa hadhi inayolingana na dhamana waliyonayo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah alimhakikishia Waziri Dk. Akwilapo kuwa shirika hilo litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kuzingatia sera na miongozo ya Serikali na kuhakikisha miradi yote inawanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, (NHC) Hamad Abdallah akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk, Leonard Akwilapo na watumishi wa shirika hilo,

Hamad amesema shirika lake linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara nchini.
Ameeleza kuwa katika utekelezaji wake, kwa mwaka 2026 NHC ilipata tuzo tatu tofauti kutokana na utendaji wake kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo gawio kwa Serikali. 

“Mwaka uliopita NHC ilipata mafanikio mbalimbali, ikiwemo tuzo tatu kutokana na utendaji bora kwenye maeneo tofauti,” amesema Hamad.

Amesema NHC kwa mwaka 2026 itajikita katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya makazi na biashara ikitambua dhima iliyonayo kutekeleza ajenda ya Serikali ya makazi bora, salama na nafuu kwa watanzania.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi