Saa wakurugenzi mashirika ya umma zahesabika
-Serikali yaja na mageuzi ya sheria
-Wana takriban siku 200 kubaki madarakani
-Mageuzi kugusa mamlaka ya Rais kuwateua
-Mashirika kusajili hisa, kuongeza wajibikaji
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Siku za wakurugenzi wa mashirika ya umma na
wakala za Serikali nchini zinahesabika, wakibakiwa na takriban siku 217 kabla
ya kujua hatma yao, iwapo watasalia au kuondoka kwenye nafasi hizo.
Kuanzia Desemba 2025, siku hizo 217 sawa na wastani wa miezi saba, zikizidishwa kwa saa 24 za kila siku moja, zinakuwa jumla ya saa 5,208, muda unaolingana na kipindi kilichosalia kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa ajira.
![]() |
| Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji |
Hatua hiyoi inakuja baada ya Serikali kutangaza mpango wa
kufanya mageuzi makubwa katika uongozi wa mashirika ya umma, unaotarajiwa
kuanza rasmi Julai 1, 2026
Kwa mujibu wa Serikali, mabadiliko hayo yatakwenda na
mabadiliko ya sheria ambapo Wakurugenzi wa mashirika watalazimika kuomba nafasi
hizo na kusailiwa badala ya kuteuliwa na Rais kama ilivyo sasa.
Mageuzi hayo ya Serikali yanakusudia kuondoa utaratibu wa
uteuzi wa moja kwa moja hasa ule unaofanywa na Rais, badala yake kuanzisha
mfumo wa upatikanaji wa viongozi kwa njia ya ushindani wa wazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa
Kitila Mkumbo, amebainisha hayo Desemba
8,2025 Dar es Salaam, akisema; “Mfumo huo mpya utaanza kutumika Julai 1, 2026, baada
ya kupitishwa kwa sheria mpya inayoandaliwa na Serikali.”
Prof. Mkumbo amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana
wa Serikali wa kuboresha utendaji wa mashirika ya umma, kujenga uaminifu wa
umma, na kuondoa malalamiko yaliyokuwapo kuhusu uteuzi wa viongozi bila
mchakato shindani.
“Kama ni Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO utaomba, uta-apply, na
utashindanishwa.
Kama unataka kuwa mjumbe wa bodi ya TPA au TISEZA utapitia
mchakato wa ushindani. Watanzania wote wenye sifa wataomba, na uchaguzi
utafanywa kwa competitive recruitment,” amesema.
Mijadala ya wanaharakati yaguswa
Kwa muda mrefu, baadhi ya wananchi, wasomi na wanaharakati
wa demokrasia nchini wamekuwa wakipendekeza kupunguzwa kwa baadhi ya mamlaka ya
Rais, ikiwemo katika uteuzi wa wakurugenzi wa mashirika na bodi za umma.
Hoja yao kuu imekuwa kwamba mamlaka makubwa ya uteuzi
huondoa ushindani wa wazi, huzuia uwajibikaji, na kuacha mianya ya upendeleo wa
kisiasa au undugu.
Mageuzi haya mapya yanayohamisha uteuzi kwenda kwenye mfumo
wa ushindani wa kitaalamu, yanaonekana kugusa moja kwa moja kilio hicho cha
muda mrefu, na kwa wengi, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha misingi ya
utawala bora na uongozi bora nchini.
Wachambuzi wa masuala ya utawala wanasema hatua hii inaweza
kupunguza minong’ono kuhusu ‘uteuzi wa kiupendeleo,’ hususan katika nyadhifa za
wakurugenzi, wajumbe wa bodi, na watendaji wa ngazi za juu katika mashirika ya
serikali.
Mabadiliko mengine yajayo
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, Prof. Mkumbo amesema Serikali inaunda mfumo mpya wa upimaji utendaji wa
mashirika ya umma, utakaozingatia tija ya kiuchumi, ubora wa huduma na mchango
wao kwenye uchumi wa taifa.
Amesema sheria mpya itayalazimisha baadhi ya mashirika ya
kibiashara ya Serikali kujisajili kwenye Soko la Hisa ili kutoa fursa kwa
wananchi kumiliki hisa, kuongeza uwazi katika uendeshaji na kuongeza
uwajibikaji kwa menejimenti na bodi.

Maoni
Chapisha Maoni