Masharti 5 kwa Polisi kukamata raia sasa ni haya
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, ameagiza Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha kuwa ukamataji wa watu unafanywa kwa kuzingatia sheria, ustaarabu na maadili ya kazi ya polisi. 
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, Desemba 8, 2025, akimwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura, kusitisha mara moja vitendo vya ukamataji wa mabavu vinavyofanywa kwa askari waliovaa kama "ninja", wasio na sare na wakiwa na silaha nzito.
Akiweka maelekezo hayo hadharani, Waziri Simbachawene amelikumbusha Jeshi la Polisi masharti matano muhimu ya ukamataji unaokubalika kisheria na unaoakisi staha ambayo ni pamoja na;
1. Askari kuvaa sare rasmi za Polisi
Waziri Simbachawene amekataza ukamataji unaofanywa na askari waliovaa mavazi kama ninja au nguo zisizowatambulisha kama polisi. Sare ni utambulisho wa kisheria na chanzo cha uaminifu kwa wananchi.
2. Ukamataji ufanyike kwa kutambulisha dhamira na sababu za Polisi
Askari wanapaswa kufika kwa staha, kujitambulisha, kueleza kuwa “Jeshi la Polisi linamhitaji mtu fulani kwa mahojiano” na kutoa maelezo yanayoeleweka. Hakuna kumvizia mtu tu bila taarifa.
3. Ukamataji ufanyike mchana kwa uwazi
Kwa mujibu wa Waziri, mtu anayefahamika makazi yake na kazini kwake hana sababu ya kukamatwa usiku au kwa misako ya mabavu. “Kwanini uende nyumbani kwake na hofu yote wakati mtu anafahamika?” alihoji.
4. Hakuna kutumia silaha nzito au kuibua hofu kwa familia
Waziri amekemea tabia ya askari kwenda nyumbani kwa raia wakiwa na silaha kubwa na kutisha watoto na familia. Ameonya kuwa kitendo hicho kinawajengea watoto chuki ya maisha dhidi ya polisi na kuacha makovu ya kisaikolojia.
5.Ukamataji lazima uendane na uzito wa kosa
Amesisitiza kuwa si sahihi kutumia nguvu kubwa au operesheni nzito kwa makosa madogo, ikiwemo malalamiko ya mtandaoni yanayopotoshwa kuwa uchochezi. “Haya mambo madogo halafu unakuja na nguvu kubwa, haya ndiyo yamefanya baadhi ya watu wawachukie polisi,” alisema.
Waziri Simbachawene amehitimisha kwa kusema kuwa Polisi ni nguzo ya amani na usalama wa wananchi, hivyo ni muhimu ukamataji ukafanywa kwa heshima, staha na kuzingatia utu ili kujenga uhusiano chanya kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Maoni
Chapisha Maoni