Prof Shemdoe: Tuhakikishe wananchi wanapata huduma bora
OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe amewataka watumishi na viongozi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa upendo, amani, mshikamano na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuwaachia tabasamu kupitia huduma hizo zinazotekelezwa na Serikali.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI katika makao makuu ya wizara hiyo Mtumba nje kidogo ya Jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwaachia Watanzania tabasamu ifikapo mwaka 2030, na kusisitiza kuwa TAMISEMI ina jukumu la moja kwa moja katika kutimiza azma hiyo.
Amesema watumishi wanapotekeleza majukumu yao katika ngazi ya mikoa, wilaya, halmashauri, kata, vijiji, mitaa na vitongoji wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zinazoendana na mahitaji yao na kuwapa tabasamu linalotarajiwa linalopaswa kuanzia kwa watumishi wenyewe kupitia utendaji uliokamilika na wa kuheshimu utu.
Prof. Shemdoe amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara hiyo, pamoja na wananchi wa Lushoto waliompa ridhaa ya kuwatumikia kama Mbunge wa Jimbo hilo.
Kwa upande wa Naibu Waziri anayeshughulikia Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Reuben Kwagilwa amesema wizara hiyo itaendelea kuongeza ushirikiano na ufanisi ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa huduma bora zinazochochea maendeleo na kuongeza tabasamu kwa wananchi.
Naye Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya Afya OWM-TAMISEMI, Dk. Jafar Seif, amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano ili kuboresha huduma za Afya hususan katika ngazi ya Afya msingi, ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.
Mapema leo, Rais Dk. Samia amewataka mawaziri wote wateule kutekeleza kwa kasi ahadi 100 za Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uhakika na kwa wakati.
Wizara ya TAMISEMI imeahidi kuendelea kuimarisha utendaji na kuwasogezea wananchi huduma bora zitakazowafanya waishi kwa matumaini na tabasamu.



Maoni
Chapisha Maoni