Mnada wa korosho waanza, Kilo Sh.3500Mtwara
-Tani 26,000 zauzwa, wakulima waanza 'kunukia' noti
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mnada wa kwanza wa zao la korosho kitaifa kwa Msimu wa Mwaka 2025/2026 umefanyika leo Novemba 8,2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba,Mtwra, huku tani 26,000 zikiuzwa kwa bei kikomo iliyokubalika na wakulima ambayo ni kati ya Sh.2,550 hadi Sh.3,520 kwa kilo moja.
![]() |
| Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile |
Bei hiyo ya msimu imekubaliwa na wakulima wa korosho wa Halmashauri za Newala na Tandahimba mkoani Mtwara kwa msimu huu, ambapo kwa mauzo ya tani hizo 26,000 katika mnada huo wa kwanza na wa kitaifa uliyofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba Newala (TANECU), wakulima wataanza 'kunukia noti' wakitarajiwa kuingiza kati ya Sh 66,300,000 na Sh91,520,000 kutegemea bei zilivyouzwa korosho hizo.
Zaidi ya tani 18,000 zilizouzwa kwenye mnada huo zimetoka Wilaya ya Tandahimba huku tani 8,000 zikitoka Wilaya ya Newala.
Kwa mujibu wa TANECO kampuni 28 kati ya 62 zilizojisajili kwa ununuzi wa korosho msimu huu wa mauzo wa mwaka 2025/2026 zimeshiriki katika ununuzi wa korosho kwenye mnada huo wa kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba,Kanali Michael Mntenjele aliyehudhuria kwenye mnada huo, na kuzungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amewataka wakulima wa korosho mkoani humo kulinda ubora wa zao hilo ili ziendelee kukidhi kiwango cha ubora katika soko na kujipatia tija zaidi, pia kulinda heshima ya taifa kimataifa.
Kanali Mntenjele amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha wakulima wanakuwa na korosho zenye ubora, kuvutia soko na kuwavutia zaidi wanunuzi kutoka katika mataifa mbalimbali.
Amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwa kuuza korosho zenye ubora wa hali ya juu na bei shindani kwa wastani wa kimataifa, ikilinganishwa na nchi zinazozalisha korosho ikiwemo Msumbiji, Brazil, Zambia na Kenya.
Huku akitoa rai kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na waendesha maghala kuwa waaminifu na kuwa wazalendo kwa kuepuka kupokea korosho chafu, Mkuu huyo wa wilaya, amesema ubora wa korosho za Tanzania, ladha nzuri ya korosho hizo na mfumo wa thabiti wa udhibiti ubora wa korosho zinazoingia sokoni, umefanya kuwa na soko la uhakika.
"Kwa kuendelea kulinda ubora, tutaendelea kuvutia wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi, tutaendelea kulinda hadhi na sifa ya korosho ya Tanzania duniani,"amehitimisha Mntenjele .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema korosho zenye ubora umhakikishia faida mkulima pia ni kulinda heshima ya taifa.

Maoni
Chapisha Maoni