Katibu Mtendaji NEEC: Vijana wekeni akiba

 

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), CPA Ben’g Issa, amewataka vijana kujiwekea akiba na kuacha tabia ya kutumia zaidi ya wanachokipata.

Ben’g ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, alipokuwa akizundua Taasisi ya Chase Your Dreams, yenye lengo la kuwa mkono wa matumaini kwa vijana wa Kitanzania, wanaopambana kufikia ndoto zao katika uchumi, elimu na ujasiriamali.

“Ukipata elfu 10, tumia elfu 5. Usitumie kupita kipato unachopata, la sivyo utakopa kwa ajili ya matumizi, wakati mikopo ni kwa ajili ya kuendeleza biashara ama uwekezaji," amesema Ben'g na kuongeza kwamba iwapo vijana wakizingatia uwekaji akiba na  kutokutumia zaidi ya wanachopata, ni wazi kuwa watafanikiwa katika mipango yao, hivyo kutimiza ndoto zao.

Katibu Mtendaji huyo wa NEEC, amesema ujio wa Taasisi ya Chase unaleta hamasa mpya ya maendeleo kwa vijana na kwamba ni imani yake baada ya miaka mitano, kundi kubwa la vijana litakuwa limefikiwa.

Beng’i  amesema Taifa la Tanzania linaweza kupiga hatua kubwa kupitia kundi la vijana, hivyo ofisi yake itaweka kipaumbele kwenye kundi hilo.

“Maendeleo ya taifa yanategemea vijana. Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi kama hizi, ili kuhakikisha vijana wanatimiza malengo yao na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla,”amesema.

Ameongeza kuwa mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa mpango, bidii na utekelezaji wa kile kinachowashinikiza ndani ya ndoto zao.

 “Ukishakuwa na ndoto, lazima uwe na mpango wa kuifanikisha. Huwezi kuota na kukaa tu. Ndoto hazijengwi kwa maneno, bali kwa vitendo na nidhamu.”

CPA Ben’g pia amewataka vijana kujishughulisha na kuacha kukaa vijiweni bika shughuli ya kufanya akieleza kuwa Serikali imedhamiria kuwawezesha vijana, ikiwemo mpango wa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, kama ilivyotajwa katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassani wakati akifungua Bunge la 13.

Amewataka vijana wasiiogope dunia ya mafanikio, akiweka bayana kuwa katika maisha kuna kushindwa na kusonga mbele, hivyo wakifeli wainuke na wasiogope kufanya mambo makubwa.

Kwa mujibu wa Ben'g uchumi ni nguzo muhimu katika heshima ya mtu kwenye jamii hata familia, kwa kuwa kukosa fedha huweza kumdhalilisha mtu kwenye ndoa, familia au katika mazingira ya kijamii.

Katibu huyo amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa kwenye serikali, ikiwemo ununuzi wa umma kwa vikundi vidogo, mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, pamoja na kushiriki katika miradi mikubwa inayotekelezwa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ChaseYour Dreams, Lightness Makondo amesema taasisi yake ilianzishwa kutokana na changamoto zinazowakabili vijana wa Kitanzania kwa kushindwa kufikia ndoto kutokana na ukosefu wa elimu sahihi, rasilimali na uongozi wa kitaaluma.

“Kila kijana ana ndoto ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii. Ndoto isipotekelezwa inabaki kuwa maono yasiyo na dira,”amesema Makondo

Amesema taasisi hiyo ilianza rasmi Machi 2024, ikiwa na program kuu tano ambazo ni After School Giving Program ambayo ilenga kutoa elimu na mwongozo kwa vijana waliomaliza shule ili kuwatengenezea dira ya maisha.

Makondo ametaja programu nyingine kuwa ni Mpango wa Kukuza Ujasiriamali ambayo inasaidia vijana kutambua fursa, kuanzisha biashara na kuzikuza kwa ujuzi sahihi.

“Pia tuna program ya Light Vikoba ambayo imejikita kwenye kuwekeza na kuweka akiba kwa vijana, ili kujenga misingi ya nidhamu ya fedha. Giving Back Program hii inarudisha kwa jamii kupitia miradi na huduma mbalimbali,” amesema.

Makondo amesema pia ipo program ya Kuwajengea Uwezo ambayo hadi sasa wamefikia vijana 1,200 ambao wamepata  mafunzo ya elimu, ujasiriamali na usimamizi wa fedha.

Makondo amesema kuanzishwa kwa wizara mpya ya vijana kutakuwa daraja muhimu kati yao na vijana katika masuala ya uchumi, elimu na maendeleo.


Mkurugezni huyo amesema Chase ni mwanga mpya kwa vijana wa Kitanzania. “Ni mwaliko wa kuamka, kuchukua hatua, kuweka mipango na kutumia fursa zilizopo ili kujenga maisha bora, uchumi imara na taifa lenye nguvu ya vijana. Ndoto hazijengwi kwa maneno zinajengwa kwa vitendo, nidhamu, mipango, na ujasiri” amesema.

Naye Joanitha Jeremiah kutoka Visionary Youth Organization amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa faida, ikiwemo kujifunza, kufanya biashara na kujenga mitandao ya maendeleo, badala ya kupoteza muda kwa malumbano, matusi na kuonyesha maisha ya kuigiza.

Wakili Fredric Usiku amewataka vijana kuacha uoga kwani unachangia hasara kubwa sana. “Ukishindwa kufanya maamuzi, utashindwa kufika unapotaka.”

Amesema ili kuwa mjasiriamali mzuri, ni lazima ujitoe kafara, ajifunze, aongeze maarifa na awe jasiri wa kuchukua hatua.

Mbunifu wa Mavazi, Feith Debora amepongeza taasisi ya Chase kwa kuwa msaada kwa vijana, kwani kwa muda mrefu vijana wamekosa msaada kutoka kwa vijana wenzake.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi