Kasi ya mageuzi, matokeo chanya miradi ya NHC kwa Watanzania
-NHC imeendelea kuutumia 2025 kuongeza kasi ya mageuzi
-Imeandika mafanikio lukuki, weledi waibeba
-Mkono wa Serikali waipa nguvu
-Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Katika ramani ya maendeleo ya Taifa, mwaka 2025 unajitokeza kama kipindi cha kipekee kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwani ni mwaka ambao kasi yake ya mageuzi imeendelea kuthibitisha kuwa si tu mtekekelezaji wa miradi ya makazi, bali ni chachu na injini ya ukuaji wa miji, uchumi wa taifa na mhimili wa ajenda ya makazi bora kwa wote nchini.
Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye
ameendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi, makazi na mipango miji, NHC
limefufua miradi iliyokwama, limezindua mikakati mipya ya uwekezaji na
limepanua kasi ya ujenzi maeneo yote ya Tanzania.
NHC iliuanza mwaka 2025 kama taasisi iliyo imara zaidi kifedha,
kiutekelezaji na kiushindani, ikibeba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya
kutengeneza Taifa lenye miji ya kisasa, yenye heshima na inayotoa fursa kwa
wananchi wote ikileta matokeo chanya.
Ushirikiano na Sekta Binafsi
Kupitia sera ya ubia iliyozinduliwa 2022, NHC limesaini mikataba
mbalimbali 21 yenye thamani ya Sh 179 bilioni na kati ya miradi hiyo, 18
tayari imepewa vibali na utekelezaji unaendelea.
NHC pia linafanya upembuzi wa viwanja 80, ambavyo vitapangiwa uwekezaji mpya wa makazi na biashara.
![]() |
| Baadhi ya majengo yaliyokarabatiwa eneo la Kariakoo |
Usimamizi wa miradi ya Serikali
NHC limeendelea kuwa mshauri elekezi na msimamizi wa miradi
ya kimkakati ya Serikali na sekta ya umma ikitenda kwa weledi.
Baadhi ya miradi hiyo ni Soko Kuu la Kariakoo (asilimia 97),
Ofisi za Wizara ya Fedha – Mtumba, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano &
Mazingira na Soko la Tanzanite – Mirerani.
Ujenzi wa majengo ya wizara nane katika Mji wa Serikali umeshakamilika
kwa zaidi ya asilimia 90 huku pia NHC ikijenga Hospitali za Kanda – Mitengo na
Musoma ambazo zimekamilika, lakini pia inajenga Jengo la TMDA Dodoma na majengo
ya TFS 44 (miradi 17), Jengo la TCRA Dodoma.
Miradi hiyo inaonesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa ndani wa
NHC katika kusimamia majengo ya viwango vya kitaifa.
Kuboresha mifumo, uwazi na ufanisi
Katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Februari 2025, viongozi wa ngazi mbalimbali wakiongozwa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, Mwenyekiti wa Bodi – Dk. Sophia Kongela na Mkurugenzi Mkuu, Hamad Abdallah walisisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kuepuka majungu kazini, kuongeza uwazi wa matumizi ya mali za umma, na kuzalisha matokeo yenye tija.
![]() |
| Baadhi ya Watendaji wa NHC wakifuatlia Mkutano mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC mwanzoni mwa mwaka huu. |
Dk. Kongela alieleza kuwa NHC linaendelea kuhakikisha uwekezaji
unaongezeka, miradi inatekelezwa kwa viwango vya juu na shirika linaendelea
kutoa gawio kwa Serikali, kiasi kinachotarajiwa kufikia Sh bilioni 6.5
mwaka huu.
Nguvu ya mageuzi
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, anasema wazi
kwamba mageuzi yaliyofanyika ndani ya miaka mitano si ya kawaida.
Kwa mara ya kwanza tangu 2016, miradi mikubwa iliyokwama
kama Morocco Square, Kawe 711 na Golden Premier Residence imefufuliwa na
kuingia hatua za mwisho baada ya Serikali kuingilia kati na kuweka mazingira
wezeshi ya ufadhili.
Matokeo ya mageuzi hayo yanaonekana kwenye hesabu ambapo
kwa miaka mitano NHC imepata faida inayofikia Sh bilioni 235.4, huku faida kwa
mwaka uliopita pekee ikifikia Sh bilioni 36.8
Katika kipindi hicho thamani ya mali za NHC hadi Juni 2024 imefikia Sh trilioni 5.5 huku kodi iliyolipwa kwa Serikali kwa miaka 5 ikiwa Sh bilioni 134.4.
![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah |
NHC katika miaka mitano imelipa gawio kwa
Serikali la takriban Sh bilioni 9.85 huku gawio la mwaka
2024/25 pekee likiwa Sh bilioni 5.5 kiasi ambacho kimeandika rekodi mpya.
Hayo si mafanikio ya kawaida bali ni uthibitisho kwamba NHC
sasa ni taasisi ya kimkakati, inayoweza kujiendesha kwa tija na kurudisha
thamani kwa umma.
Ujenzi unaobadilisha taifa
Katika kipindi cha miaka mitano, NHC imejenga nyumba
5,399 zenye thamani ya Sh bilioni 659.5 na kati ya hizo 3,217
zimekamilika huku 2,182 zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Ni nyumba zinazoanzia Dar es Salaam hadi Tanga, kutoka
Dodoma hadi Kagera – kila mahali NHC imeacha alama.
NHC ina miradi mikubwa ya kimkakati ambayo tayari
imetekelezwa au inaendelea ambayo ni pamoja na Morocco Square – Dar es
Salaam, Kawe 711 Housing Project – Dar es Salaam,Samia Housing Scheme –
Kijichi & Kawe, Golden Premier Residence – Dar es Salaam, 2H Plaza –
Morogoro na Mkwakwani Project – Tanga.
Mingine ni 2F Project – Singida, Soko la Madini
la Tanzanite – Mirerani, Meru Shops – Arusha, Samia Iyumbu Apartments – Dodoma,
Njendengwa Housing – Dodoma.
Zaidi ya hapo, Shirika la Nyumba la Taifa limetimiza
mikataba 67 ya kazi za umma yenye thamani ya Sh bilioni 458.2, ikiwa ni
pamoja na Jengo la Ofisi za Wizara Dodoma, Kitengo cha Moyo cha JKCI na Soko la
Kimataifa la Tanzanite Mirerani.
NHC pia limeanzisha miradi ya ubia 21 na sekta
binafsi yenye thamani ya Sh bilioni 351.
Tabora Commercial Complex
Katika mji wa kihistoria wa Tabora, NHC imeanzisha mradi wa
Tabora Commercial Complex, jengo la kwanza la kisasa kuwahi kujengwa
mkoani humo – thamani Sh bilioni 4, kukamilika Aprili 2026.
Ni mradi unaoonekana kama kuhuisha urithi wa Utemi wa
Milambo–Tabora kuondoka katika unyonge na kujiweka kwenye ramani ya miji ya
kisasa.
Zaidi ya maombi 200 ya nafasi za biashara, ofisi na
makazi yamepokelewa kabla hata jengo kukamilika.
Ushirikiano na sekta binafsi
Katika ziara yake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, NHC iliwasilisha taarifa ya mwelekeo wa 2025, ikionyesha kuwa NHC inatekeleza miradi inayozingatia Dira ya Taifa, miradi inajaa ubunifu, thamani ya fedha na tija ya kijamii, ujenzi unaenda sambamba na mahitaji ya miji inayoendelea kukua.
Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC, Mhandisi Godwin Maro,
alieleza kuwa NHC linafanya zaidi ya kujenga majengo, linaboresha maisha,
uchumi, ajira na mazingira ya miji.
Dodoma
Mradi wa Samia Iyumbu Apartments unategemewa kutoa nyumba
zaidi ya 300, zenye miundombinu ya Barabara,maji na umeme, shule na huduma
za afya
Eneo la Njendengwa, NHC inaendelea kujenga nyumba zaidi ya 120
kwa watumishi wa umma na sekta binafsi.
Dar es Salaam
Mtanda Commercial Complex (iliyofikia zaidi ya asimilia
75 kukamilika, wenye thamani ya Sh bilioni 4.2
Samia Kijichi Housing Scheme
Nyumba zaidi ya 300 za gharama nafuu, zenye huduma
muhimu na mazingira tulivu zinajengwa.
Samia Housing Scheme – Kawe
Nyumba 560 zilizokamilika na nyingine 560
zinazofuata.
Ni mradi wa thamani ya Sh bilioni 48 ukiwa sehemu ya mpango wa nyumba 5,000
wenye thamani ya Sh bilioni 466.
Miradi hiyo kwa inabadilisha sura ya jiji na kutoa makazi ya hadhi kwa maelfu ya watu.
Miradi ya upembuzi, ukarabati
NHC pia linafanyia ukarabati majengo ya zamani, kuziwekea mifumo
mipya ya maji, umeme wa kisasa, barabara za ndani, mandhari na bustani mpya
Hatua hiyo inalinda thamani, kupandisha ubora wa miji na kuongeza mapato ya Serikali.
Tuzo na utambuzi
Utekelezaji wa kiwango bora na usimamizi wa fedha za
Serikali umeiweka NHC katika ramani ya kutambuliwa kitaifa na kupata tuzo.
Katika kikao kazi cha viongozi wa mashirika ya umma kilichofunguliwa na Makamu wa Rais,(Sasa mstaafu), Dk. Philip Mpango Agosti 2025, NHC lilipata Tuzo ya Shirika Bora la Umma kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Vigezo vilivyozingatiwa katika kupewa tuzo hiyo ni pamoja
na uzalishaji wa mapato, ukwasi, faida, ubora wa taarifa za fedha, ufanisi wa
huduma kwa jamii na utekelezaji wa hoja za CAG.
Ushirikiano na sekta ya fedha
Ziara ya kitaalamu ya Benki ya ABSA katika miradi ya
Kijichi na Kawe ni uthibitisho wa ubora
wa kazi za NHC.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ABSA, Obedi Laiser, amesema; “Tumeshuhudia kwa macho yetu ubora wa kazi ya NHC. Hii ni kazi inayochangia kupunguza uhaba wa makazi, kukuza ajira na kuinua hadhi ya miji yetu.”
![]() |
| Baadhi ya Wafanyakazi wa Benki ya ABSA wakiwa na watendaji wa NHC hivi karibuni |
Kwa NHC, huu ulikuwa mhuri wa ubora kutoka kwa sekta ya fedha.
Kwa mwaka huu 2025, NHC imekuwa mshirika madhubuti
wa maendeleo ya Taifa kutoka ujenzi wa nyumba, masoko ya madini,
majengo ya biashara, hadi kubuni miradi ya ubia na kujenga miundombinu
endelevu, ikiendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini na weledi.
Kwa kufanya hivyo, NHC imepanua ajira, imeongeza makusanyo
ya kodi na gawio kwa Serikali, imechochea ukuaji uchumi wa wananchi, imebadilisha
sura ya miji na imejenga heshima na matumaini mapya kwa Watanzania.
Kwa kasi ya utekelezaji, uwajibikaji na ubunifu
unaoendelea, NHC linaibuka kama nguzo ya Taifa katika sekta ya makazi,
likielekea kutimiza ndoto ya Tanzania yenye makazi bora, salama na yenye hadhi
kwa wote.









Maoni
Chapisha Maoni