Historia yaandikwa: Dk. Mwigulu achukua mikoba ya Uwaziri Mkuu

 -Watumishi wa Umma kwenda kwa gia ya kupanda mlima

-Aahidi usawa kwa watanzania wote

-Akumbuka umasikini alioishi, kubeba zege

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Alhamisi ya Novemba 13,2025 itabaki kuwa ya kukumbukwa kwa Dk. Mwigulu Nchemba na Bunge la Tanzania baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwasilisha bungeni jina la mbunge huyo wa Iramba Magharibi, Mkoa wa Singida, akimteua kuwa Waziri Mkuu atakayeongoza shughuli za Serikali Bungeni.

Waziri Mkuu Mteule, Dk.Mwigulu Nchemba

Uteuzi huo wa Rais Samia ni hatua moja mbele katika kuunda Serikali yake, baada ya uteuzi wa kwanza wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.

Takriban dakika tano tangu kuanza kwa kikao cha Bunge cha leo, ambapo  saa 3:06 mpambe wa Rais aliruhusiwa kuingia bungeni na kuiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, bahasha kutoka kwa Rais iliyokuwa na jina pendekezwa la Waziri Mkuu, ilipofunguliwa lilisomwa jina la Nchemba mbele ya wabunge ambao baadaye watamthibitisha kwa kura 369 kati ya 371, kura 2 zikiharibika.

Waziri Mkuu Mteule, Dk. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuapishwa kesho saa4 asubuhi Ikulu, Chamwino Dodoma akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Kassim Majaliwa.

Majaliwa ametumikia nafasi hiyo kwa miaka kumi mfululizo, kuanzia mwaka 2015 hadi 2025.

Akitoa salam za shukrani kwa Bunge baada ya kuthibitishwa, Waziri Mkuu huyo Mteule, amemshukuru Rais Samia kwa kumteua kushika wadhifa huo na Bunge kwa kuonesha imani naye kwa kumthibitisha, huku akiahidi kufanya kazi kwa kutoa nafasi sawa kwa wabinge wa pande zote za walio wengi na walio wachache.

Kuhusu uongozi wake kwa nafasi ya Waziri Mkuu, mteule huyo ameahidi kila mtanzania kupata nafasi sawa katika utoaji huduma, akitilia mkazo uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kufanya kazi kwa weledi.

Amesema licha ya utajiri wa taifa, bado asilimia 8% ya Watanzania wanaishi katika umaskini wa kupindukia na asilimia 26% wanaishi kwa mlo mmoja.

Wazir Mkuu Mteule amesema hana taarifa hizo kwa kuzisoma tu kwenye vitabu, bali kwa kuzishuhudia mwenyewe kupitia maisha aliyokulia kijijini kwa takribani miaka 32.

“Mimi umaskini wa Watanzania sijausoma kwenye vitabu, nimeuishi. Mheshimiwa Spika, katika miaka takribani 32, nimepitia maisha ya umaskini, maisha ambayo nilikuwa najifunika nguo aliyokuwa anajifunga shemeji yangu,” amekumbuka Dk. Nchemba akisimulia.

Ameeleza kuwa ilimbidi asubiri shimeji yake huyo amalize kazi zake usiku, ndipo yeye aipate na kujifunika, lakini pia adamke asubuhi, ili awahi kuirudisha ili shimeji yake ajifunge akafanye kazi zake.

Amesimulia kuwa katika maisha yake baada ya kuhitimu masomo yake, alifanya kazi ya kubeba zege, huku mkewe akiwa mama ntilie katika eneo hilo alipobeba zege, hivyo anafahamu ugumu wa maisha hayo. 

Waziri Mkuu Mteule huyo amebainisha kuwa safari iliyo mbele yake katika Uwaziri Mkuu inahitaji nguvu ya ziada akisema;“Watumishi wa Umma na Watanzania wote, lazima twende kwa gia ya kupandia mlima; lazima twende kwa gia ya kupita bahari yenye mawimbi na anga lenye mawingu ili chombo kifike salama.”

Ametahadharisha akisema: “Wote walio wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania tuwe tayari, nitakuja na fyekeo na rato. Maono ya Mheshimiwa Rais lazima yatekelezwe.”

Katika hatua nyingine, Dk. Nchemba, amepokelewa na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwenye makazi ya Waziri mkuu, Mlimwa jijini Dodoma leo Novemba 13, 2025 baada ya kuthibitishwa na Bunge.


 

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi