INEC yataja wabunge viti maalum, majina ya vigogo yachomoza

-Wamo wakongwe, waliobeba majina ya wanasiasa wakongwe

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),imetangaza majina 115 ya wabunge wa Viti Maalum iliowateua kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 huku majina ya wabunge wakongwe wa viti maalum, wakiwamo pia wapya vijana wenye 'unasaba' na wanasiasa maarufu nchini na viongozi wastaafu.

Katika majina hayo 115 yaliyotangazwa na INEC, Chama Cha Mapinduzi(CCM), kilichotwaa kiti cha Urais kupitia aliyekuwa mgombea wake Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dk. Emmanuel Nchimbi, kikipata viti 113 na Chauma kikipata viti viwili. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025, ulifanyika Oktoba 29.

Akizungumza wakati wa kutangaza majina hayo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele, amesema; "Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake kilichofanyika leo tarehe 07 Novemba, 2025 imefanya uteuzi wa Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu 115 kati ya idadi ya Wabunge 116 wanaopaswa kuteuliwa."

Hata hivyo Jaji Mwambegele amesema nafasi ya Mbunge mmoja uteuzi wake utafanyika baada ya kukamilisha uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Fuoni –Tanzania Zanzibar na Jimbo la Siha Tanzania Bara.

"Uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 66(1)(b) na 78(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 zikisomwe pamoja na kifungu cha 112 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024",amesema wenyekiti wa INEC. 

Baadhi ya majina ya vigogo wa waliorejea kupitia viti maalum ni pamoja na Pindi Chana, Mary Chatanda na Najma Giga, Maryprisca Mahundi, Salome Makamba, Bonna Kamoli,Cecilia Paresso na Stela Ikupa.

Kwa upande wa wateule wanaobeba majina makubwa ya wanasiasa walioshika nyadhifa mbalimbali za uongozi nchini ni pamoja na Halima Bulembo, Zainab Rashid Kawawa, Jacqeline Chrisant Mzindakaya, Janeth Peter Pinda, Lucy Similya Kombani na Jesca John Magufuli.  

Ikumbukwe kuwa Abdalla Bulembo aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Marehemu Rashid Kawawa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na Waziri Mkuu wa Tanzania, wakati Mzindakaya amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa na Merehemu Celina Kombani amewahi kuwa Waziri, huku Mizengo Pinda akiwa Waziri Mkuu mstaafu na Hayati John Magufuli alikuwa Rais wa Tanzania. 

Makundi hayo ya wabunge wazoefu na vijana yanatajwa kuweza kuwa na Bunge bora zaidi, litakaloijenga pia CCM imara zaidi, ikizingatiwa kuwa na mchanganyiko wa vijana waliolelewa kwenye maadili ya uongozi ya watangulizi, pamoja na wakongwe, hivyo kuongeza kasi ya maendeleo ya taifa, hasa vijana.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele (katikati) akiongoza kikao cha Tume kilichokutana Jijini Dodoma leo Novemba 7, 2025 na kupitisha majina ya wabunge wa viti maalum. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume , Jaji wa Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk na kushoto ni Katibu wa Tume ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ramadhani Kailima. 
INEC ikiwa katika kikao chake hii leo. 

Orodha ya Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu 115 walioteuliwa ni kama ifuatavyo;






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi