Papa Leo XIV: Uhuru wa kidini ni nguzo ya amani duniani
-Alipongeza Shirika la Misaada kwa Kanisa kwa Kutetea Uhuru wa Kidini
Roma, Italia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Leo XIV amesema vitendo vya uhasama na vurugu dhidi ya watu wanaoshikilia imani na mitazamo tofauti, wakiwemo Wakristo vinaongezeka duniani na kwamba hakutakuwa na amani bila uhuru wa dini.
![]() |
| Papa Leo wa XIV akibariki msalaba wakati wa mkutano na shirika la Aid to the Church in Need (CAN)Oktoba 10, 2025. |
Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa kauli hiyo katika hotuba yake
alipokutana na wanachama wa shirika la kipapa Aid to the Church in Need
International (CAN), ambao umefanyika Oktoba 9-2025, siku chache kabla ya
kuchapishwa kwa Ripoti ya Uhuru wa Kidini Duniani itakayozinduliwa rasmi
Oktoba 21 mwaka huu.
Akinukuu maneno ya Papa Francis, Papa Leo amesema,
“Hakutakuwa na amani bila uhuru wa dini, uhuru wa kufikiri, uhuru wa kujieleza,
na heshima kwa maoni ya wengine.”
Alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki linatetea uhuru wa kidini
kwa watu wote, akirejelea tamko la Mtaguso wa Pili wa Vatikano lililosisitiza
kwamba uhuru wa kidini ni haki inayopaswa kutambuliwa na kila taifa.
Amesema kuwa uhuru wa kidini ni nguzo ya jamii kwa sababu
unalinda nafasi ya kimaadili inayomwezesha mwanadamu kutumia dhamiri yake kwa
uhuru
“Uhuru huu unamwezesha mtu binafsi na jamii kutafuta
ukweli, kuuishi kwa uhuru, na kuushuhudia waziwazi,” amesema na kuongeza;
“Uhuru wa kidini si
haki ya kisheria tu au upendeleo tunaotunukiwa na serikali, ni hali ya msingi
inayowezesha upatanisho wa kweli.”
Baba Mtakatifu LeoXIV ameonya kwamba uhuru wa kidini unapominywa,
jamii huingia kwenye hatari ya kushuhudia kuvunjika kwa uhusiano wa kimaadili
na kiroho.
Katika hotuba yake, Papa Leo XIV amerejea kwamba ziara ya
wanachama wa ACN mjini Roma inafanyika wakati ambapo kunaongezeka kwa vitendo
vya uhasama na vurugu dhidi ya watu wanaoshikilia imani na mitazamo tofauti,
wakiwemo Wakristo.
“Utume wa ACN unasimama kinyume na hali hiyo ya vurugu na Kanisa
haliwezi kamwe kuwaacha ndugu na dada zetu wanaoteswa kwa ajili ya imani yao,”
amesema Papa Leo XIV.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani, amesisitiza kwamba;
“Haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa kidini “si hiari bali ni haki ya msingi,”
akiongeza kuwa kila binadamu hubeba ndani yake “tamaa ya kina ya kutafuta
ukweli, maana ya maisha na ushirika na wengine pamoja na Mungu.”
Ameeleza kuwa uhuru wa kidini umejengwa juu ya heshima ya
utu wa mwanadamu, aliyeumbwa kwa sura ya Mungu na kupewa akili na uhuru wa
kuchagua.
Papa Leo amekumbusha kuwa Aid to the Church in Need
ilianzishwa mwaka 1947 kama mwitikio wa mateso ya vita, lengo likiwa kukuza
msamaha na upatanisho, huku likitoa sauti kwa Kanisa popote linapoteseka au
kutishiwa.
Alisifu Ripoti ya Uhuru wa Kidini Duniani
inayochapishwa kila baada ya miaka miwili, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu ya
kuongeza uelewa na kufichua “mateso yaliyofichika ya watu wengi.”
Papa pia aliwashukuru wanachama wa ACN kwa msaada wao wa
kifedha kwa taasisi za Kanisa duniani kote, hasa katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati, Burkina Faso, na Msumbiji.
“Popote ambapo Aid to the Church in Need inajenga
upya kanisa, inasaidia watawa, au inasaidia kituo cha redio au usafiri,”
alisema, “mnatia nguvu maisha ya Kanisa na muundo wa kiroho na kimaadili wa
jamii.”
Papa Leo XIV alihitimisha kwa kusema kuwa msaada kwa
Wakristo wa ndani unawasaidia wachache hao kuwa wajenzi wa amani katika nchi
zao, wakawa “ishara hai ya maelewano ya kijamii na undugu, wakionyesha kwa
majirani zao kuwa dunia tofauti inawezekana.”

Maoni
Chapisha Maoni