Majaliwa: Bila walimu hakuna wataalam, hakuna viongozi wa kesho
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote hapa duniani kwani ndio wanaotoa rasilimali watu yenye elimu ambayo ni muhimu zaidi kwa Taifa.
![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
Amesema hayo
Oktoba 03, 2025 katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, yaliyofanyika Bukombe mkoani Geita kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ushirombo.
Majaliwa amesema kwamba mafanikio ya kielimu, kijamii na kiuchumi hutokana na juhudi za walimu kwa kuwa walimu ni fahari ya familia, jamii na taifa na kupitia mikono yao vijana wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi na maadili ya uzalendo.
“Kila hatua ya ustawi wa kijamii na kiuchumi huanzia darasani, kupitia juhudi na maarifa ya walimu. Bila walimu, hakuna taaluma, hakuna viongozi wa kesho na hakuna Taifa linaloweza kusimama imara, walimu ndio chimbuko la uvumbuzi na ubunifu wa kizazi kipya,” amesema Majaliwa.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa kada ya ualimu nchini, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kada hiyo, ikiwemo kuwapandisha madaraja walimu na kuimarisha mafunzo kwa walimu.
![]() |
Walimu wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani iliyofanyika mkoani Geita Oktoba 3, 2025. |
Amebainisha kwamba ili kukabiliana na upungufu wa walimu nchini, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuthamini na kuwekeza katika kada ya ualimu kwa kuajiri walimu wapya kila mwaka.
Katika hotuba yake. Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Ofisi ya Rais – UTUMISHI kufanya mgawanyo wa walimu ndani ya mikoa husika kwa kuhakikisha kila shule inapata walimu ili watoto wa Kitanzania wapate elimu bora.
“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Vyuo vya Ualimu na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imarisheni mafunzo ya kitaaluma na endelevu kwa walimu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya dunia ya leo,”amesisitiza Majaliwa.
Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amesema kuwa taaluma ya ualimu ni taaluma pakee inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu wenyewe na wakati wowote hujinyima muda wake na nguvu zake zote kumtengeneza mtu kuwa mume au mke bora au hata mzazi bora.
![]() |
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko |
“Taaluma ya ualimu humfanya mtu kuwa raia mwema kwenye nchi na zaidi sana humfanya kuwa mtumishi, mfanyakazi na mzalishaji mali bora, wakati wote wa maisha yake, hii ni taaluma ambayo tunaamini ni ya uumbaji wa pili baada ya mwanadamu kuzaliwa na wazazi wake, kazi ya pili huendelea hapa duniani na muumbaji huwa ni mwalimu,” amesema Dk. Biteko.
Ameongeza kuwa Mwalimu ndiye anayetoa mwelekeo wa maisha ya kila mtu na ukiona jamii yoyote yenye ustaarabu na kustaarabika huhitaji kupiga ramli kujua nani chanzo chake bali mwalimu ndio sababu yake.
Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo ameeleza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya shughuli mbalimbali zinazowawezesha walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya ikiwemo ujenzi wa miundombinu shuleni na lengo ni kukuza ujifunzaji na ufundishaji.
"Serikali inathamini jitihada zinazofanywa na walimu, wao wamekuwa kiini cha mafanikio. Tukumbuke kila mmoja wetu amepita kwenye mikono ya walimu, tunawashukuru,".
Maoni
Chapisha Maoni