Trump atimua kazi maelfu ya watumishi wa umma
Washington, Marekani. Serikali ya Rais Donald Trump nchini Marekani, imetangaza kuwaachisha kazi maelfu ya wafanyakazi ikiwa ni sehemu ya mpango wake mkubwa wa kupunguza wafanyakazi, unaohusiana na kufungwa kwa taasisi za Serikali.
![]() |
Rais Donald Trump wa Marekani |
Ofisi ya Usimamizi na Bajeti ya nchi hiyo (OMB) imeeleza katika
hati za mahakama kuwa notisi ya kuachishwa kazi zimetumwa kwa takribani
wafanyakazi 4,200 katika wizara na taasisi za serikali nane.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Forbs leo, hatua hiyo iliyoanza
jana Oktoba 9-2025, inafuatia kesi iliyofunguliwa na Shirikisho la Wafanyakazi
wa Serikali ya Marekani (AFGE), chama kikubwa zaidi cha wafanyakazi wa Serikali
kinachowakilisha wafanyakazi 800,000 kufungua kesi ikipinga wafanyakazi hao
kuachishwa kazi.
Kwa mujibu wa OMB, karibu wafanyakazi 1,500 wa Wizara ya Fedha
ya Marekani wameachishwa kazi, wakiwemo takribani wafanyakazi 1,300 kutoka
Mamlaka ya Mapato ya Marekani (IRS), kama ilivyoripotiwa na Bloomberg.
Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu (Health and Human
Services Department) pia imeathirika kwa kiwango kikubwa na hatua hiyo, ambapo
OMB imeripoti kuwa takriban wafanyakazi 1,200 wameachishwa kazi.
Awali, Gazeti la The New York Times, liliripoti kuwa makumi
ya wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi katika Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia
Magonjwa (CDC) wamepokea barua za kuachishwa kazi siku ya jana Oktoba 9-2025,
wakiwemo takribani maofisa 70 wa Huduma za Uchunguzi wa Magonjwa ya Mlipuko
(Epidemic Intelligence Service) na baadhi ya wafanyakazi wa jarida la Morbidity
and Mortality Weekly Report.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Wizara ya Usalama wa
Ndani (Department of Homeland Security) imewajulisha wafanyakazi 176 kwamba
wataachishwa kazi, wote wakiwa ni watumishi wa Wakala wa Usalama wa Mtandao na
Miundombinu (Cybersecurity and Infrastructure Security Agency), kama
ilivyoripotiwa na PBS.
Maelezo kuhusu hatua hizo za kuwaachisha kazi yametolewa
hadharani Ijumaa jioni jana, muda mfupi baada ya Mkuu wa Bajeti wa White House,
Russ Vought, kutangaza kupitia mtandao wa X kwamba “mchakato wa kupunguza
wafanyakazi umeanza.”
Baada ya tangazo hilo, Chama cha Wafanyakazi wa AFGE kilifungua haraka ombi
mahakamani kikipinga hatua hiyo na kutaka izuiliwe mara moja.
Maoni
Chapisha Maoni