ABSA, NHC waandika historia mpya ya makazi Tanzania

 - Benki ya ABSA yatembelea miradi ya kisasa ya NHC Dar es Salaam

 - NHC yajengea wataalam ABSA uelewa, kuwezesha umiliki nyumba bora

 - Ushirikiano sekta ya fedha, ujenzi matumaini mapya ya makazi endelevu

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Ni asubuhi tulivu ya Ijumaa Oktoba 10, mwaka 2025. Magari kadhaa yenye nembo ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na Benki ya ABSA Tanzania, yakipenya barabara za Jiji la Dar es Salaam, kuelekea kwenye miradi miwili mikubwa ya makazi inayotekelezwa na NHC, ambayo ni Samia Housing Scheme eneo la Kijichi na Kawe 711 Housing Project.

Lengo la safari hiyo limewekwa wazi kuwa ni kujifunza, kushirikiana, na kujenga daraja kati ya sekta ya fedha ikiongozwa na ABSA kwa upande mmoja na NHC upande wa sekta ya ujenzi.

Timu ya wataalamu wa ABSA imefanya ziara hiyo ili kujionea kwa macho ubora wa kazi ya NHC, kubaini fursa za biashara, lakini  zaidi ya yote, kufahamu jinsi mikopo ya nyumba inavyoweza kumsaidia Mtanzania wa kawaida kutimiza ndoto ya kumiliki makazi yake ya kisasa.

Walipowasili Kawe, upepo wa baharini ulipuliza taratibu, ukipenyeza kwenye majengo mapya yaliyosimama kwa Fahari yakiwa na urefu wa kipekee eneo hilo, Kawe 711 Housing Project ilionekana kama sura mpya ya makazi ya kisasa kutokana na majengo yaliyosimama kwa mpangilio, yakionesha ubunifu na usanifu wa kisasa unaokidhi viwango vya kimataifa.

Msafara huo kisha ukaelekea Kijichi, kwenye Samia Housing Scheme, mradi unaolenga Watanzania wa kipato cha kati na cha chini  eneo lililojaa matumaini, nyumba bora zenye gharama nafuu na mazingira tulivu ya familia.

“Tumeshuhudia kwa macho yetu ubora wa kazi unaofanywa na NHC,” anasema kwa msisitizo Mkurugenzi Mtendaji wa ABSA Tanzania, Obedi Laiser na kuongeza;
“Nyumba hizi ni za kisasa kabisa,  zinadhihirisha ubunifu na weledi wa hali ya juu. Hii ni kazi inayochangia kupunguza uhaba wa makazi, kukuza ajira na kuinua hadhi ya miji yetu.”

Kauli yake inapokelewa kwa tabasamu na nyuso za furaha kutoka kwa wenyeji wao NHC. Kwa NHC ziara ya ABSA imekuwa ni ishara ya kuthamini kazi yao, ambayo hasa imejikita katika dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na nafuu.

“Miradi hii ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Serikali kuhusu makazi endelevu,” ameeleza Mhandisi Grace Musita, Meneja wa Miradi wa NHC Kijichi.

Anafafanua;“Tunatumia teknolojia za kisasa zinazopunguza gharama na kulinda mazingira. Tunataka kila Mtanzania awe na nyumba bora bila kuathiri uwezo wake wa kifedha.”

Akizungumzia zaidi mradi wa Kijichi Msita anasema unatarajiwa kuwa na majengo Matano yenye nyumba 260 zitakazokuwa za chumba kimoja cha kulala, vyumba viwili, vyumba vitatu na maegesho ya magari takriban 300, ambapo pia litajengwa jengo litakalokuwa na maeneo ya maduka na huduma mbalimbali za kijamii.

Mhandisi Msita anabainisha; “Ujenzi wa mradi huu tayari umeanza kutekelezwa Agosti 22, mwaka huu 2025 na utakamilika Agost 22 mwaka 2027 takriban miaka miwili kufikia ukamilifu wake, ambapo thamani yake ni shilingi bilioni 41.5.”

Anabainisha kuwa bei kwa nyumba ya chumba kimoja ni shilingi milioni 112, vyumba viwili vya kulala ni shilingi milioni 220 na vyumba vitatu vya kulala ni shilingi milioni 335 ikijumuishwa na VAT.

“Malipo yapo ya namna tattu, kuna malipo kwa fedha taslimu, kuna malipo kwa awamu kuanzia walau asilimia 10 ya bei, lakini pia mnunuzi anaweza kununua kwa mkopo wa benki, (Mortgages),” anasema Msita.

Kwa macho ya ABSA, falsafa yao ya “Hadithi yako ina thamani” imepata maana halisi wakati wa ziara hiyo. Kwa benki, kila nyumba iliyoonekana kwenye miradi ya NHC imekuwa ni hadithi ya mafanikio, hadithi ya familia itakayopata amani, heshima, na mwanzo mpya kwa kupata nyumba za NHC.

Katika mazungumzo yaliyofuata, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa NHC, Deogratious Batakanwa anasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya pande hizo akisema:

“ABSA imekuwa mshirika wetu muhimu sana. Wametuwezesha kifedha kwenye ujenzi wa miradi hii na wamekuwa daraja kwa wateja wetu kupata mikopo ya nyumba. Huu ni mfano bora wa sekta binafsi na umma kushirikiana kwa manufaa ya Watanzania.”

Ziara hiyo haikuwa tu tukio la kiserikali, bali pia ilikuwa ni sura hai ya matumaini mapya.

Kwa upande wa uchumi, miradi ya NHC inaongeza ajira, biashara ndogo ndogo hata za kati, na thamani ya ardhi katika maeneo yanayozunguka miradi hiyo. 

Kijamii, miradi ya NHC inatoa makazi salama na yenye heshima, ikibadilisha maisha ya wananchi kutoka kukaa nyumba za kupanga hadi kuwa wamiliki kamili.

Kupitia ushirikiano kama huu, ndoto ya umiliki wa nyumba inakuwa halisi zaidi, hasa Benki kama ABSA zinapotoa mikopo nafuu, na taasisi kama NHC zikijenga nyumba bora hivyo, mafanikio yanakuwa ya pamoja.

Hatimaye msafara wa ABSA uliondoka Kijichi ukiwa umebeba zaidi ya kumbukumbu. Umehitimisha ziara hiyo ikibeba imani mpya katika uwezo wa sekta binafsi na umma kuleta mabadiliko chanya.

NHC na ABSA Tanzania wameonyesha kuwa maendeleo jumuishi hayaji kwa maneno pekee, bali kwa vitendo, kwa kuweka msingi imara wa jamii yenye makazi bora, salama na ya kisasa kwa kila Mtanzania.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi