NHC na urithi wa Mwalimu Nyerere: Miaka 26 ya kuendeleza ndoto makazi bora kwa kila Mtanzania
- NHC chini ya Rais Dk. Samia imefufua falsafa ya utu ya Mwalimu Nyerere
- Miaka 26 tangu kifo cha Baba wa Taifa, NHC inaendelea kuwa nguzo ya heshima, maendeleo na utu kwa Watanzania wote
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Kila inapowadia
tarehe 14 Oktoba, Watanzania hukusanyika kwa heshima na kumbukizi ya maisha na
kazi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ikumbukwe kuwa
Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya St. Thomas
Jijini London
Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Ni siku inayobeba
hisia nzito, si tu kwa sababu aliongoza harakati za ukombozi, bali pia kwa sababu
alisimamia maono ya kujenga taifa lenye utu, heshima na usawa.
Miongoni mwa
mambo yaliyokuwa karibu sana na moyo wake ni suala la makazi bora aliamini
kwamba mtu hawezi kuishi kwa heshima bila nyumba salama na yenye hadhi.
Kutokana na
falsafa hiyo, mwaka 1962 Nyerere akiwa kiongozi wa Serikali ya Tanganyika
(baadaye Tanzania) alianzisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia Sheria
ya Bunge Na. 45.
Lengo lilikuwa
wazi, kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora.
Mwalimu Nyerere akishiriki kuchimba msingi wa nyumba za NHC Magomeni miaka ya 1963 wakati wa operesheni ondoa makuti.
Nyerere
alisisitiza kwamba taifa changa haliwezi kusimama imara kama wananchi wake
wataendelea kuishi katika makazi duni.
Hivyo, NHC likawa sehemu ya urithi wake wa kijamii, chombo cha kuendeleza utu na mshikamano wa WatanzaniaMiaka ikasonga, changamoto za kiuchumi na kisera zikajitokeza, lakini azma haikupotea. Kufikia miaka ya 1990, mageuzi makubwa yalifanyika, na NHC likapewa uwezo wa kujiendesha kibiashara huku likidumisha wajibu wake wa kijamii.
Mageuzi haya
yakaliweka Shirika kwenye ramani kama taasisi thabiti, yenye uwezo wa
kushirikiana na sekta binafsi na kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa.
Katika kipindi
cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Samia Suluhu Hassan, NHC limepata mwanga mpya wa ufanisi na ubunifu.
Mwalimu Nyerere ( katikati) akikagua nyumba za magomeni zilizojengwa na NHC miaka ya 1963 wakati wa operesheni ondoa makuti.
Kupitia dira yake ya uwekezaji na ubia, miradi mikubwa ya nyumba imezinduliwa, ikiwemo Samia Housing Scheme inayolenga kujenga nyumba 5,000 kote nchini.
Tayari nyumba 560 za awamu ya kwanza Kawe zimekamilika na zote kuuzwa hata kabla ya ujenzi kukamilika, hii ni ishara ya uhitaji mkubwa na imani ya wananchi kwa NHC.
Hii ni pamoja na ukarabati na ujenzi
upya wa Soko la Kariakoo ambalo limeshakamilika, Jengo la Ofisi ya Wizara ya
Fedha na Mipango kwa asilimia 95, Jengo la Makamu wa Rais – Mazingira kwa
asilimia 90 na Soko la Madini la Tanzanite Mirerani kwa asilimia 100.
Katika uendelezaji wa sera ya ubia,
NHC liliboresha sera yake mwaka 2022, likiunga mkono sera ya ufunguaji
uwekezaji iliyoasisiwa na Rais Samia. Hadi sasa mikataba 21 yenye thamani ya
Shilingi Bilioni 179 imesainiwa, na miradi kadhaa iko katika hatua mbalimbali.
Katika eneo la Kariakoo pekee,
nyumba 172 zilizokuwa zimevunjwa zitatekelezwa upya na kuibua zaidi ya nyumba
2,100 za kisasa za makazi na biashara.
Shirika pia
limeleta mageuzi makubwa katika ujenzi wa miradi ya kibiashara na ya kijamii.
Mradi wa Morocco Square jijini Dar es Salaam ni mfano hai: asilimia 100 ya
nyumba za makazi zimeuzwa, maduka yote yamepangishwa, na hoteli yenye vyumba 81
sasa inatoa huduma.
Miradi mingine kama Kawe 711, Kahama Plaza, Masasi Plaza na Mtanda Commercial Building mkoani Lindi uliokamilika kwa asilimia 93, na 2H Commercial Building mkoani Morogoro uliokamilika kwa asilimia 99 yakiakisi ubora wa usimamizi wa kisasa.
Kwa upande wa
ukandarasi, NHC limepewa jukumu kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kitaifa,
ikiwemo majengo ya Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, Shule ya Uchumi ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hospitali ya Kanda ya Kusini – Mitengo, na
Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Musoma.
Matokeo ya kazi
hii yote yanaonekana wazi: mapato ya Shirika yamepanda, mali zake zimeongezeka
hadi kufikia zaidi ya trilioni 5, na wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya
kumiliki nyumba kupitia mikopo ya muda mrefu inayotolewa kwa kushirikiana na
benki zaidi ya 22.
Miaka 26 tangu tumuage Mwalimu Nyerere, urithi wake bado unaishi kupitia NHC. Kila jengo jipya linaloinuka, kila familia inayopokea funguo za nyumba, na kila mji unaopata sura mpya ni ishara kwamba ndoto ya Baba wa Taifa inaendelea.
Kwa hakika, NHC
si tu shirika la nyumba, bali ni sehemu hai ya historia, falsafa na ndoto ya
kujenga taifa lenye utu, usawa na maendeleo endelevu.
x




Maoni
Chapisha Maoni