NHC yapata tuzo maalum vigezo vitano vikiibeba
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetunukiwa tuzo maalum, baada ya kuibuka kuwa moja ya mashirika ya umma yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2023/24.
Tuzo hiyo imetolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika
hafla rasmi iliyofanyika kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji
Wakuu wa Taasisi za Umma, kilichofunguliwa rasmi Agosti 2,2025 na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, jijini Arusha.
Tuzo hizo zilizingatia vigezo vya kiuendeshaji ikiwamo ukuaji
wa mapato ya ndani, kuboresha ukwasi, rejesho la uwekezaji, udhibiti wa
matumizi na kuimarisha faida.
Vigezo vingine ni kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali,
ufanisi katika matumizi, utekelezaji wa hoja za kikaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uchapishaji wa taarifa za fedha, na maboresho
ya utoaji huduma kwa jamii.
Taasisi nyingine zilizotunukiwa tuzo maalum zilitangazwa
chini ya makundi manne mahsusi kulingana na aina na majukumu husika huku NHC likiwa
katika kundi la mashirika yanayofanya
biashara, ambapo tuzo zilitolewa kwa
mashirika yaliyoboresha mapato, faida, ukwasi na rejesho kwa mtaji wa Serikali.
Pamoja na NHC katika kundi hilo wengine walioshinda ni Bohari ya Dawa (MSD) na Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO).
Maoni
Chapisha Maoni