BRELA ilivyojizatiti utoaji elimu, kusimamia Sheria ya Miliki Bunifu

- Usajili wapaa

- Miliki Bunifu 7 zasajiliwa kila siku ndani ya siku 365 

- Hataza 30

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umejidhatiti kutoa elimu kwa wananchi, wasanii, wabunifu, watafiti na taasisi mbalimbali nchini kuhusu umuhimu wa kulinda na kusajili bunifu, sambamba na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Miliki Bunifu.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo(aliyeketi kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa kuhusu utendaji BRELA.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao, kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Miliki Bunifu nguzo ya maendeleo

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Miliki Bunifu Duniani yaliyofanyika Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dk. Selemani Jafo amesisitiza umuhimu wa wabunifu, wajasiriamali na wasanii kusajili bunifu zao ili kulinda haki zao kisheria.

Waziri Jafo amesema kauli mbiu ya mwaka huu, “Miliki Bunifu na Muziki: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu,” imelenga kuhamasisha wasanii na wabunifu wa sekta mbalimbali kutambua kwamba bunifu ni mali kama mali nyingine.

“Usajili wa bunifu ni hatua muhimu ya kuhakikisha wabunifu wananufaika na kazi zao wakiwa hai, na hata baada ya kufariki warithi wao watanufaika. Serikali imeweka mifumo thabiti ya ulinzi ili kuhakikisha ubunifu unaleta tija kwa Taifa,” amesema Jafo.

Aidha, ameuelezea mpango mkubwa wa Serikali wa kujenga viwanda 9,048 nchini kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwishoni mwa 2025 hadi mwaka 2031, akisema unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya vijana milioni 6.5, ambapo bunifu na miliki bunifu vitakuwa nyenzo muhimu katika ustawi wa viwanda hivyo.

Elimu ya Miliki Bunifu vyuo vikuu, taasisi za utafiti

BRELA imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa vyuo vikuu, vyuo vya ufundi na taasisi za uzalishaji kuhusu umuhimu wa kulinda bunifu kupitia usajili wa hataza na alama za biashara.

Akizungumza Aprili 16, 2024 katika Chuo cha Waislamu Morogoro (MUM), Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa BRELA, Loy Mhando, alieleza:

“Bunifu nyingi katika vyuo zinatokana na tafiti za wanafunzi na wahadhiri. Tunahimiza bunifu hizi zisajiliwe ili walinziwe kisheria na ziweze kuwanufaisha wabunifu na jamii kwa ujumla.”

BRELA imetoa elimu katika vyuo mbalimbali vikiwemo;Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), TaSUBa – Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo,Chuo cha Mafunzo ya Ufundi VETA, SIDO na Innovation Hub ya Taasisi ya Afya Ifakara (TAOTIC).

Lengo la BRELA kutoa elimu hiyo ni kuwajengea wabunifu uwezo wa kulinda bunifu zao, kupanua masoko na kupata manufaa ya kifedha kupitia tafiti na uvumbuzi.

Loy Mhando

Sauti za Wanufaika

Mmoja wa walionufaika na usajili wa Miliki Bunifu kutoka Kampuni ya TALANTA, Ronald Nakaka anasema kwa kusajili wa ubunifu unamwezesha kufanya kazi zake hadi nje ya Tanzania bila kikwazo kwani sheria ya kimataifa inampa ulinzi wa kazi zake hasa za sanaa ya muziki.

Anawahimiza watanzania hasa wajasiriamali vijana kusajili bunifu zao hatua inayoweza kuwafikisha kwenye ndoto zao kimaisha.

Siku ya Kimataifa ya Miliki Bunifu

Kila mwaka, BRELA hushiriki kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Miliki Bunifu lengo likiwaa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kusajili bunifu.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, wadau kutoka COSOTA, BPRA, COSOZA, vyuo vikuu, wajasiriamali na wasanii walishirikishwa, huku BRELA ikiendesha warsha na mikutano ya wadau kujadili mikakati ya kukuza uelewa wa usajili wa bunifu na kuongeza ubunifu wenye tija kwa Taifa la Tanzania.

Ushirikiano na wadau

BRELA ilivyotoa elimu kwa wadau wake, taasisi za elimu na wajasiriamali kuhusu Miliki Bunifu.

Katika eneo hilo BRELA imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo; COSOTA (Ofisi ya Hakimiliki Tanzania, BPRA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar) COSOZA, Taasisi ya Utafiti wa Mbegu, taasisi za teknolojia na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO).

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa ya ulinzi wa bunifu, ikiwemo rasimu ya Mkataba wa Sheria ya Maumbo na Michoro Bunifu iliyojadiliwa Novemba 2024 jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Mchango wa vyombo vya habari

Vyombo vya habari nchini vimekuwa mshirika muhimu wa BRELA katika kutoa elimu kwa umma.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile

Katika warsha iliyoandaliwa na BRELA kwa wahariri, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliwataka wahariri kuwa mabalozi wa elimu ya miliki bunifu:

“Baada ya kupata elimu hii, tunapaswa kuwafikishia Watanzania taarifa sahihi kuhusu miliki bunifu, umuhimu wa usajili na namna ya kunufaika na kazi zao,” ameeleza Balile.

BRELA inahimiza vyombo vya habari kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Faida za kusajili bunifu

Kwa mujibu wa BRELA, usajili wa bunifu unatoa manufaa kadhaa, ikiwa ni pamoja na:

  • Ulinzi wa kisheria dhidi ya wizi au uvunjaji wa haki.
  • Fursa ya kupata mikopo kupitia taasisi za kifedha.
  • Kuongeza thamani ya bidhaa na huduma kwa kutumia alama za biashara.
  • Kupanua masoko ya kitaifa na kimataifa.
  • Kuwezesha wabunifu kufaidika kifedha na kazi zao.

Kupitia mikakati yake ya utoaji elimu, ushirikiano na wadau, na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa bunifu, BRELA imejidhatiti kuhakikisha wabunifu, wasanii, watafiti na wajasiriamali nchini wanatambua thamani ya bunifu na kunufaika nazo.

Serikali imesisitiza kuwa, ifikapo mwaka 2030, miliki bunifu itakuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.

Changamoto

Hata hivyo, zipo changamoto zinazowakabili watanzania katika kulinda  Miliki Bunifu na Hataza. Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Miliki Bunifu na Hataza(WIPO) , baadhi zikiwa ni ukosefu wa uelewa kuhusu Miliki Bunifu, Kushindwa kutekeleza Sheria ya Miliki Bunifu na Udhibiti mdogo wa matumizi yasiyo rasmi ya Miliki Bunifu na Hataza.

Msaada kwa wajasiriamali, wabunifu, wasanii

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa,(Pichani chini), amewataka wasanii, wabunifu na wajasiriamali kusajili majina ya bidhaa na huduma wanazotoa kupitia brand zao ili kuyalinda kisheria.

Godfrey Nyaisa
Kwa mujibu wa Nyaisa, usajili unawawezesha wabunifu kupata haki ya kipekee ya kutumia bunifu zao na kuzuia mtu mwingine kuziiga au kuzitumia kibiashara bila ridhaa yao. Aidha, unatoa fursa ya kukopesheka katika taasisi za kifedha kwa kuwa BRELA inatoa vyeti vinavyotambulika kisheria. 

BRELA inavyoboresha mifumo

Nyaisa anabainisha kwamba BRELA imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaboresha mifumo ya usajili Miliki Bunifu na Hataza kwa kuanzisha mfumo wa usajili mtandaoni, Kuwezesha maombi wa njia rahisi na  kutoa mwongozo wa watumiaji.

Naye Dk. Ashatu Kijaji, Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, amewataka wanawake wajasiriamali kusajili bunifu na biashara zao ili kuongeza thamani ya bidhaa na kulinda haki zao kisheria.

“BRELA inazilinda bunifu na biashara kisheria. Iwapo mtu ataiga kazi yako, una haki ya kumshtaki na BRELA itasimama kukutetea,” amesema Nyaisa kwa niaba ya Dk. Kijaji.

Wadau kulinda bunifu kimataifa

BRELA, kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), imeandaa rasimu ya Mkataba wa Sheria ya Maumbo na Michoro Bunifu inayolenga kuweka mfumo wa kimataifa wa kulinda bunifu.

Nyaisa, anasema kuwa sheria hiyo itakapopitishwa, wabunifu wa maumbo, vifungashio, mavazi na michoro mbalimbali watapata fursa ya kulinda bunifu zao katika nchi nyingi kwa kutumia ombi moja tu kupitia WIPO.

“Hii itapunguza gharama za ulinzi wa bunifu na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za wabunifu wa Kitanzania katika soko la kimataifa,” anasema.

Hali ilivyo, muda na hatua za usajili

Akizungumzia hali ya usajili miliki bunifu ilivyo kwa sasa, Ofisa Usajili kutoka BRELA, Stanlaus Kigosi anaeleza kuwa kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo mwamko wa watu kusajili kazi zao unavyoongezeka.

“Usajili sasa unachukua nafasi, mwamko unaongezeka kila siku. Hii inatokana na BRELA inavyoendelea kujitahidi kuwafikia wajasiriamali, vikundi vya wanawake, hata kutoa elimu kwenye vyuo vikuu na taasisi mbalimbali,” anasema Kigosi, huku akibainisha kwamba takwimu kamili za Miliki Bunifu zilizosajiliwa zipo nje ya uwezo wake.

Anafafanua kuwa katika usajili wa Miliki Bunifu, usajili wa Alama za Biashara unafanyika zaidi kuliko usajili wa Hataza, jambo linalotokana asili ya maeneo hayo mawili.

Wakati Alama za Biashara huweza kuchukua muda mfupi kubuniwa na kuwasilishwa BRELA kwa usajili, HATAZA uhitaji muda zaidi kutokana na kuhusisha zaidi Teknololojia ya Habari(IT), hivyo pia kuhitaji kuidhinishwa na taasisi au bodi husika kabla kuziombea usajili w Miliki Bunifu.

Kuhusu muda wa usajili Miliki Bunifu, Kigosi anabainisha kuwa usajili hufanyika na kukamilika ndani ya siku 90, ukijumuisha masuala mbalimbali ya kisheria na kanuni ndani nan je ya nchi, ikiwemo kufanyia uchunguzi Miliki Bunifu inayoomba kusajiliwa, kuitangaza kwa siku 60 ndipo husajiliwa ikiwa haikuwekewa kipingamizi.

Gharama usajili Miliki Bunifu

Akihitimisha maelezo yake, Kigosi anasema usajili wa Miliki Bunifu unaenda sanjari na kulipia gharama kwa mujibu wa sheria.

 “Miliki Bunifu husajiliwa kwa kulipiwa gharama ambayo ni Shilingi 130,000. Gharama hiyo ni nafuu ikilinganishwa na zinazotozwa na nchi nyingi za Ukanda wa Afrika Mashariki,” anasema Kigosi.

Takwimu  Miliki Bunifu

Akizungumza na mwandishi wa Makala haya, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Jamii wa BRELA, Joyce Mgaya ameeleza kuwa mamlaka hiyo ina Idara maalum inayokusanya na kuhifadhi takwimu za masuala mbalimbali yanayosimamiwa na  kutekelezwa na BRELA ikiwemo Miliki Bunifu na Hataza.

“Katika mwaka mmoja uliopita, BRELA imesajili Miliki Bunifu  takriban 2,615. Lakini pia Hataza zilizosajiliwa katika muda huo ni 30,” anasema Joyce.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara, wajasiriamali kuzingatia sheria za nchi kwa kusajili Miliki Bunifu zao na Hataza, ili kuendana na matakwa ya kisheria, lakini pia kunufaika ya usajili huo ambao ni ulinzi kwa ubunifu na ugunduzi wao.

Serikali na Sera mpya ya Miliki Bunifu

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma (Mwana FA), anasema Serikali ipo mbioni kukamilisha Sera ya Miliki Bunifu itakayotoa mwongozo mpya wa ulinzi na usimamizi wa haki za wabunifu nchini.

“Maendeleo ya taifa yanategemea bunifu. Miliki bunifu zitaongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” anasema Mwinjuma.

Sera hiyo itatoa mwanga kwa wabunifu kupata mikopo, kufikia masoko makubwa zaidi na kunufaika na ubunifu wao kikamilifu.

Kwa jitihada zake na kujitambua, BRELA inaendelea kujidhatiti na kuwa nguzo ya ulinzi na uendelezaji wa bunifu nchini. Inafanya hivyo kupitia elimu, ushauri, sera na ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Ushindi wa BRELA katika kuwezesha utekelezaji wa Sheria ya Miliki Bunifu ni Ushindi wa Watanzania

Taasisi hiyo inalenga kuweka mfumo imara wa kuhakikisha wabunifu, wajasiriamali, wasanii na vyuo vikuu wananufaika na ubunifu wao.

Kwa usajili wa bunifu, Tanzania inalenga kuongeza kipato cha wabunifu, kukuza sekta ya viwanda, kupanua soko la kimataifa na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi