Rais Samia ahimiza kudumisha amani, haki kuelekea Uchaguzi Mkuu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema upo umuhimu wa
kuhakikisha Taifa linaendelea kudumu katika misingi imara ya haki, amani, umoja
na mshikamano wa kitaifa iliyowekwa na waasisi wa Tanzania , akieleza kwamba ili
kudumisha misingi hiyo ushirikiano na mshikamano wa viongozi wa dini ni nguzo
muhimu.Rais Dk. Samia akizungumza katika Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Ameeleza hayo katika hotuba yake leo Agosti 24, 2025 kwenye Kongamano
la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambalo liliandalia na Umoja wa
Maimamu Tanzania (UMATA) na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania.
Taarifa Ikulu iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano
ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu imeeleza kuwa Rais Dk. Samia amesema uchaguzi ni
fursa ya kidemokrasia inayopaswa kwenda sambamba na kulinda amani na utulivu wa
taifa.
“Kudumisha amani ni
utamaduni wetu tuliojijengea katika demokrasia ya uchaguzi. Tuendeleze
utamaduni huu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu,” amesema Rais Dk. Samia.
Amebainisha kuwa kipindi cha uchaguzi huongeza joto la
kisiasa, lakini amani itaendelea kudumu ikiwa viongozi wa dini, kijamii na
kisiasa watashirikiana kuhubiri amani na mshikamano kwa kuepusha migongano
isiyo ya lazima.
Kuhusu nafasi ya wadau mbalimbali katika kudumisha amani
wakati wa uchaguzi, Rais Dk. Samia amewataka wanasiasa kuepuka lugha za
uchochezi katika kampeni, badala yake
kujikita katika sera na hoja.
Rais Dk. Samia pia ameeleza umuhimu wa kuzingatia maelekezo
ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), pamoja na kutoa ushirikiano kwa
vyombo vya ulinzi na usalama, huku akikumbusha
nafasi muhimu ya vyombo vya habari katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa hasa
katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Waandishi wa habari ni kundi muhimu kwa mustakabali
wa amani ya nchi yetu. Kalamu zao zinaweza ama kudumisha au kuhatarisha amani
ya nchi yetu,” amesema Rais Dk. Samia.
Amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi
Mkuu Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa kushiriki kupiga kura ni wajibu wa
kikatiba na kizalendo unaojenga mustakabali wa taifa.
.
Maoni
Chapisha Maoni