Wafanyakazi wa majumbani wamwangukia Rais Samia -
-Wamwomba aridhie Mkataba wa ILO kuwaokoa taabuni
Mwandishi
Wetu, daimatznews@gmail.com
Serikali ya Rais
Samia Suluhu Hassa, imeombwa kukamilisha mchakato wa kuridhia Mkataba wa
Kimataifa wa Kazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 189 na kupitisha ili
kuwezesha haki za msingi za wafanyakazi wa majumbani.Rais Samia Suluhu Hassan
Ombi hilo
limetolewa na wafanyakazi wa majumbani, wakieleza kuwa mkataba huo wa kazi
zenye staha utawasaidia kupata haki na kuheshimiwa kama wafanyakazi wa sekta
nyingine.
Wametoa ombi hilo
walipokuwa wakizungumza katika Kikao Kazi kilichowakutanisha kwa siku mbili mjini
Morogoro, ambapo wamepata Mafunzo ya Utatuzi wa Migogoro ya Wafanyakazi wa Majumbani.
Mwenyekiti wa Wafanyakazi
wa Majumbani Tanzania, Zanini Athuman anasema mkataba huo wa ILO unaweka wazi
stahiki halali kwa wafanyakazi wa majumbani, ikiwemo kupewa mapumziko ya
kutosha, kuishi katika mazingira ya heshima (hasa kwa wanaoishi kwa waajiri).
“Pamoja na uwepo
wa sheria mbalimbali hapa nchini zinazolitambua kundi hilo, bado kuna ugumu
katika utekelezaji wake, kutokana na sheria kutoruhusu nyumba ya mtu binafsi
kuwa ofisi ya kazi. Mwarobaini pekee unaotazamiwa ni kuridhiwa kwa mkataba huo,”
amesema Zanini.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhini, Mahotelini, Huduma
za Kijamii na Ushauri (CHODAWU) Said Wamba, amewahimiza wafanyakazi wa
majumbani kujiunga katika vyama mbalimbali vya wafanyakazi, ili kuwa na sauti
ya pamoja ya kupambania haki na stahiki zao.
“Tunajaribu
kuwainua hawa wafanyakazi wa majumbani, wapo chini mno, hili si jambo la
CHODAWU pekee, bali jamii nzima ya Watanzania ina jukumu la kufanya kuwaokoa
kwa sababu wanafanya kazi kubwa na muhimu kwa waajiri wao na taifa kwa ujumla,
lakini hawapati matunda ya jasho lao,”amesema Wamba.
Shirika la Kazi
Duniani (ILO) limewakutanisha kwa pamoja mkoani Morogoro Tume ya Usuruhishi na Uamuzi
(CMA) Taasisi ya Serikali inayohusika na utatuzi wa migogoro ya kazi Tanzania Bara
pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi wa majumbani katika kikao kazi cha siku
mbili, lengo likiwa kutafuta mwarobaini wa pamoja wa kukabiliana na changamoto
zinazolikumba kundi hilo muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Mmoja wa
washiriki wa mafunzo hayo, Desdelia Saimon, amesema kuchelewa kwa mchakato wa
kuridhia mkataba huo kunawafanya waendelee kufanya kazi katika mazingira
hatarishi, ikiwemo ukosefu wa haki ya faragha na maisha binafsi pamoja na kinga
ya kisheria ya kutosha.
Naye Nasra
Seleman kutoka Dar es Salaam amesema; “Endapo Serikali itaridhia mkataba huo, utatufungulia
mambo mengi kwa sababu, mkataba huo unatuhusu moja kwa moja sisi wafanyakazi wa
majumbani. Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aridhie mkataba huo ili na sisi
tutendewe haki kama wafanyakazi wengine.”
Awali, akizungumza
katika ufunguzi wa kikao hicho, Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Utambuzi na Mazingira
ya Kazi kwa Wafanyakazi wa Majumbani kutoka ILO, Chiku Semfuko amesema kwamba mafunzo
hayo yatawawezesha wafanyakazi wa majumbani kutambua mahali sahihi panapofaa kupeleka
migogoro yao na kupata utatuzi.
Naye Mkurugenzi
na Mtendaji Mkuu CMA Tanzania Bara, Usekelege Mpulla, amesema tayari mwongozo
maalumu wa utatuzi wa migogoro ya wafanyakazi kwa ajili ya wafanyakazi wa
majumbani pekee umeshaandaliwa, lengo likiwa kutafsiri utatuzi wa migogro pamoja
na kutekeleza matakwa ya kisheria pamoja na mkataba wa ILO namba 189.
“Tumejipanga
kuhakikisha haki za wafanyakazi wa majumbani zinatolewa kwa wakati na mafunzo
haya yatakapokamilika, tunaamini wasuluhishi wanaohusika na migogoro watapata
uwezo wa kumaliza migogoro kwa haraka,” amesema Mpulla.
Awali, Kamishna Msaidizi
Idara ya Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,
Rehema Moyo aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mafunzo hayo amesisitiza CMA
kuhakikisha wanatoa kipaumbele kushughulikia migogoro ya wafanyakazi wa
majumbani kutokana na ugumu wa mazingira ya kazi wanayopitia kupata stahiki
zao.
“Ni muhimu pia
hata wafanyakazi wenywe wa majumbani wajue haki zao. Pamoja na kuwa vyombo vya
kisheria vipo, lakini lazima wapewe
elimu wa kutambua wapi waende kupata utatuzi wa migogoro yao,” amesema.
Baadhi ya wafanyakazi
majumbani waliohudhuria mafunzo hayo walieleza umuhimu wa Serikali kuridhia na
kuupitisha Mkataba Namba 189 wa ILO.
Summary:
Kuridhiwa kwa mkataba namba189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ni hatua muhimu
ya kuwapa wafanyakazi wa majumbani hadhi, heshima na ulinzi wanaostahili katika
mazingira yao ya kazi. ucheleweshaji wa mchakato huo huendelea kuwafanya
wafanyakaizi wa majumbani kufanya kazi katika mazingira hatarishi huku wakikosa
mikataba rasmi, mapumziko, haki ya faragha na kinga ya kisheria
Mwisho.
Maoni
Chapisha Maoni